BERLIN,UJERUMANI

KANSELA wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa mabadiliko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema umoja huo unapaswa kubadilika ili uweze kukabiliana na changamoto za dunia za karne ya 21.

Hayo aliyaeleza katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa.

Kansela huyo alisisitiza kuwa Ujerumani iko tayari kutimiza majukumu yake, na itafurahi zaidi ikiwa majukumu hayo yatajumuisha kiti chake cha kudumu katika Baraza la Usalama lililo pana zaidi.

Katika ujumbe huo, Kansela Merkel alisema ubora wa Umoja wa Mataifa lazima uakisi matakwa ya wanachama wake.

“Nchi yoyote inayodhani inaweza kuendelea peke yake inajidanganya”, alisema Kansela Merkel bila hata hivyo kuitaja nchi yoyote kwa jina.