CONGO DRC

WAWAKILISHI wa makundi 70 yenye silaha waliokutana huko Murhesa katika eneo la Kabare, karibu na mji wa Bukavu, katika Mkoa wa Kivu Kusini, wametia saini mkataba wa kusitisha mapigano.

Nakala ya mwisho ilitiwa saini baada ya siku tatu za mazungumzo yaliyoandaliwa na mashirika matatu yasiyo ya kiserikali yaliyobobea katika utatuzi wa migogoro.

Mkataba huo unaeleza uundwaji wa kamati za ufuatiliaji zitakazohusika na kutathmini kuheshimu mkataba wa usitishwaji wa mapigano na kutengeneza ramani za maeneo yenye ukosefu wa usalama kwa kutambua wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo husika.

“Tumesaini mkataba wa kusitisha uhasama, lakini hii sio mara ya kwanza tunasaini mkataba kama huo. Tunasaini mkataba wa kusitisha mapigano na siku inayofuata uhasama huo unaanza tena. Ninaamini kwamba sote tumechoka vita”.

Vita katika milima huko Fizi, sio suala la wanamgambo tena kama mnavyoamini, ni serikali iliyoingilia kati huko na ndiyo inayosaidia kundi la Mai-Mai, kwa kulipa silaha na vifaa.

Nadhani ikiwa serikali inajiamini, uhasama huu utasitishwa moja kwa moja. Kama serikali itaamua kutulinda, wapiganaji wa kundi la Twirwanehowako tayari kuweka silaha chini, ” amesema Muhamiriza Jean-Scohier, msemaji wa kundi la Twirwaneho, linalopiga kambi katika eneo la Fizi.

Muungano wa makundi ya Mayi-Mayi uitwao Biloze Bishambuke, unaopiga kambi pia katika eneo la Fizi, umefutilia mbali tuhuma hizo.

Kuongezeka kwa makundi yenye silaha kunachangia kwa kuzorota kwa hali ya usalama katika mkoa wa Kivu Kusini. Kutoka makundi 38 mwezi Desemba na kufikia leo makundi karibu 70, hasa kwa sababu ya mgawanyiko kutokana na malumbano ya ndani.