NA HUSNA SHEHA
MWANAFUNZI mmoja wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka tisa jina linahifadhiwa wa Skuli ya Msingi ya Mahonda, amenusurika kubakwa baada ya kupata msaada wa wasamaria wema huko Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.
Akizungumza na mwandishi wa Zanzibar leo , Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Shaaban Sarboko Makarani, alisema mwanafunzi huyo alikuwa akitokea kwa mjomba wake na kuelekea skuli, ndipo alipomkuta Juma Haji Ali anaekisiwa kuwa na umri wa miaka 25 mkaazi wa Mahonda Mazizini.
Alisema baada ya kijana huyo kumuona mwanafunzi huyo alimkamata na kumpeleka ya nyumba anayoishi kwa lengo la kutaka kumbaka.
“Baada ya kumuingiza ndani alianza kumvua nguo za ndani na kuanza kumchezea sehemu zake za siri kwa lengo la kutaka kumbaka, lakini yule mtoto alipiga kelele na majirani kusikia na kwenda kuvunja mlango na kumtoa”alisema.
Alisema baada ya hapo wananchi walimuweka mtuhumiwa chini ya ulinzi na kupeleka ripoti Skuli ambayo anasoma mwanafunzi huyo.
“Hapo ndipo wasamaria wema walimchukuwa mtuhumiwa na kumpeleka katika kitengo cha dawati la jinsia kwa lengo la kuchukuliwa hatua za kisheria”alisema.