NA KHAMISUU ABDALLAH

MSHITAKIWA Asma Shaaban Abdalla (30) mkaazi wa Nyerere bado anaendelea kufika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake inayomkabili.

Agosti 22 mwaka huu mshitakiwa huyo alifikishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na kesi yake ya shambulio la kuumiza mwili kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mohammed Haji Kombo aliiomba mahakama kuhairishwa kesi hiyo na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi akiwemo mlalamikaji.

Hakimu Mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Subeit alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 14 mwaka huu.

Mwanamama huyo anakabiliwa na mashitaka mawili tofauti ikiwemo la shambulio aliyodaiwa kuyatenda Julai 1 mwaka jana saa 4:00 asubuhi huko Magomeni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alidaiwa kuwa bila ya halali alimshambulia Bahati Mustafa Hassan kwa kumpiga makofi na ngumi mwilini na kumsababishia kupata maumivu mwilini mwake.

Mwendesha Mashitaka Wakili Mohammed alidai kuwa kosa la pili alilotenda mshitakiwa huyo ni kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu cha 326 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Asma alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo aliharibu mashine ya kupondea unga pamoja na kuvunja vikombe mali ya mlalamikaji Bahati jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo yupo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana aliyopewa mahakamani hapo kesi yake ilipofikishwa kwa mara ya kwanza na kuomba kupatiwa dhamana ambayo alipewa ya kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 100,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja alimdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maanshi waliowasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi.