NA HUSNA SHEHA

SHEHA wa Shehia ya Kibweni Subira Haji Yahya, amewataka wananchi shehia hiyo kuchukua tahadhari ya maradhi ya malaria kwa kuweka usafi wa mazingira katika maeneoa yao wanayoishi, ili kuepusha mazalia ya mbu.

 Hayo alisema huko Ofisini kwake Kibweni wakati alipokuwa akiwapa elimu hiyo wanashehia hiyo kutokana na kuzuka upya maradhi hayo katika shehia hiyo.

Alisema shehia yake imekuwa na wagonjwa wa malaria sita ambao walifanyiwa uchunguzi mwezi wa Julai mwaka jana hadi Juni 2020 .

Aidha, aliwashauri wananchi hao kuondosha vichaka sambamba na kusafisha makaro  na madimbwi yasio rasmin na kuacha kutupa taka katika sehemu zisizo rasmin, ili kuepusha mazalia ya mbu ambao ndiyo chanzo cha maradhi hayo na amewataka watumie chandarua.

Nao wananchi hao akiwemo Mwandawa Suleiman, wamempongeza sheha huyo kwa kuwapa elimu hiyo ,na kuahidi kwamba watajitahidi kuyatunza mazingira sambamba na kuondosha vichaka, ili kuepusha mazalia ya Mbu ambayo ni chanzo cha maradhi hayo.