SOKA ni mchezo unaopendwa na mashabiki wengi duniani na ndiyo unaotajwa kupewa kipaumbele zaidi ya michezo mingine.

Pamoja na soka kupendwa, lakini kumekuwa hakuna mwamko mkubwa katika mchezo huo kwa upande wa wanawake, badala yake kumekuwa na hamasa kubwa kwa wanaume pekee.

Kwenye programu nyingi za mchezo wa soka nchini, soka la wanawake limekuwa halipewi umuhimu na wakati mwengine jinsia hiyo hubaguliwa licha ya kuwepo walio na vipaji.

Kwa sasa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limekuwa na vipaumbele kwenye soka la vijana na wanawake na hiyo imesababisha mashirikisho mengi ya soka kuendesha ligi za wanawake.

Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kwenye sekta ya michezo, kwa sasa imekuwa ikiimarisha soka la wanawake na kwa mara nyengine, ligi ya wanawake imeendelea kuchezwa ambapo jumla ya timu tano zinashiriki.

Pamoja na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kuendesha ligi hii katika wakati mgumu, ipo haja ya kuendelea kuungwa mkono zaidi ili kuiwezesha ligi hiyo kufanikiwa.
Zanzibar Leo tukiwa miongoni mwa jamii ya wanamichezo, tunaona ipo haja ya kuifanya ligi ya wanawake iwe bora na yenye ushindani ili kukuza kiwango cha soka la wanawake.

Ni ukweli usiopingika kwamba soka la wanawake bado halijawa na nguvu na hiyo imesababisha hata timu za wanawake kutokuwa vizuri na zenye kufahamika.

Hivyo, ipo haja ya kuweka mikakati kwenye soka la wanawake na kupatiwa uungwaji mkono wa kutosha kama ilivyo kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar na tuna imani kuwa ligi hiyo nayo itakuwa na ushindani na bora ili kuiwezesha kutoa timu imara ya taifa itakayopeperusha vyema bendera kimataifa.

ZFF iendelee kupambana katika kuona ligi ya wanawake inachezwa na kupewa aina fulani ya msukumo, licha ya kutambulika kuwepo kwa changamoto kubwa katika suala la wadhamini.

Ni wakati wa wadau wa soka visiwani hapa kuungana na ZFF kuhakikisha ligi ya wanawake inachezwa katika mazingira mazuri na yatakayochochea wasichana wengi zaidi kupenda kucheza mchezo huo.

Wapo wasichana wengi wenye vipaji ambao wanaona aibu kujitokeza, lakini kama kutawekwa mazingira rafiki, bila ya shaka vipaji vingi vitajitokeza na kuunganisha nguvu ya pamoja kwenye soka la wanawake kwa maslahi ya taifa.
Kila heri la Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake Zanzibar.