WASHINGTON,MAREKANI

KIMBUNGA Sally kimepiga mwambao wa karibu na mpaka baina ya majimbo ya Alabama na Florida Kusini mwa Marekani, kikiambatana na mafuriko na upepo unaokwenda kwa kasi ya km 165 kwa saa.

Mamia ya watu walilazimika kuokolewa baada ya nyumba zao kujaa maji.

Kimbunga hicho kilisomba maboti yaliyokuwa ufukweni na kuyatupa nchi kavu, na kuangusha miti na kuezua nyumba katika miji ya Pensacola na Mobile.

Nyumba zipatazo 540,000 za makaazi ya watu na biashara ziliachwa bila umeme katika eneo hilo la kaunti ya Escambia, ambako maofisa walisema watu 377 waliokolewa kutoka nyumba zilizofurika maji, ikiwemo familia ya watu wanne ambao walikuwa wamepanda mitini kuepuka kumezwa na mafuriko.

Hali ya hatari ilitangazwa katika baadhi ya miji ya mwambao katika jimbo la Alabama, wakati vikosi vya kitaifa vya uokozi vikisubiriwa kuwasili katika majimbo yaliyoathiriwa.