BAMAKO,MALI

KIONGOZI wa kijeshi nchini Mali, Kanali Assimi Goita ametaka taifa lake kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, ambavyo vimewekwa baada ya mapinduzi ya mwezi uliopita katika taifa hilo masikini la Sahel.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Mali Goita alisema uteuzi wa hivi karibuni wa rais wa mpito raia, unamaanisha kwamba viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi lazima wasitishe marufuku yao ya kufanya biashara na Mali.

Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi yenye mataifa15 wanachama ECOWAS mpaka wakati huu haijasema lolote lakini Ufaransa, ambayo ina vikosi vyake kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi nchini Mali, imeupokea vyema uteuzi wa waziri wa zamani wa ulinzi Bah Ndaw na viongozi wengine wa mpito kama hatua yenye kutia moyo.

ECOWAS, iliifunga mipaka ya mataifa yake na Mali na kuweka vikwazo, baada ya jeshi la Mali Agosti 18, kumuondoa madarakani rais Boubacar Keita.