NA LAYLAT KHALFAN
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema imeandaa mpango maalum wa mradi wa kituo cha daladala cha kisasa katika eneo la Kijangwani Mjini Zanzibar.
Kamishana wa Idara wa Uchumi na miradi ya mashirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi PPP, Rahma Salim Mahfudh, aliyasema hayo katika kikao cha kusikiliza maoni ya wananchi juu ya mradi huo kikao ambacho kilifanyika ofisi za UMAWA Kijangwani Mjini Zanzibar.
Alisema azma ya serikali ni kuimarisha miundombinu ya jamii na kuleta mabadiliko katika nchi ambapo kituo hicho kitakua na sehemu ya kushushia na kupakia abiria pamoja na ujenzi wa maduka na ukumbi utakaotumika kwa shughuli za kijamii.
Aliwasisitiza wananchi hao kujitahidi kutunza na kuthamini juhudi za serikali ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa huku wakiamini kuwa serikali ipo kwa ajili ya kuwatatulia shida zao na kuwajengea misingi bora ya upatikanaji wa maendeleo.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wananchi , walisema mradi wa ujenzi huo utakaokua wa kihistoria ambao utaweza kuleta mafanikio ndani ya nchi pamoja na ukuaji wa uchumi.
Mmoja ya wananchi hao, Hassan Daudi Ismail ,mkaazi wa eneo la Kijangwani, alisema kuwepo kwa kituo hicho kitaweza kuimarisha na kukuza biashara zao kwa kujipatia kipato kwa haraka kitakachoweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Said Juma Ahmada, alisema wakati umefika kwa wananchi kuunga mkono miradi inayoanzishwa na serikali katika kuleta maendeleo ya haraka nchini, kwani anaamini mradi huo endapo utaanza wananchi wengi watapata ajira kwa kuweza kuendesha shughuli zao mbalimbali katika eneo hilo.