NA MWANAJUMA MMANGA

FAINI ya shilingi 1, 000,000 imemshukia kijana wa miaka 26 aliyedaiwa kufanya makosa manne ikiwemo kutengeneza mifuko ya plastiki katika kiwanda cha ZATEA kiliopo Mwakaje Wilaya ya Magharib ‘A’.

Kijana huyo ni Nassor Said Saleh, ambae amshitakiwa katika Mahakama ya mwanzo Malindi chini ya Hakimu  Mwanaidi Abdalla Othman, ambapo mshitakiwa huyo pia alipatikana na kosa la kufanya biashra  ikiwa hana leseni.

Maelezo hayo yalisomwa na Mwendesha Mashitaka, Suleiman Khalfan Masoud, alidai kuwa mshitakiwa huyo pia alipatikana na kosa la kutengeneza mikate katika kiwanda hicho pamoja na kumiliki mifuko ya kuhifadhia mikate jambo ambalo ni kinyume na sheria nambari 7 ya mwaka 2014, sheria ya Zanzibar.

Aidha Suleiman, alidai kuwa mshitakiwa huyo alishitakiwa kwa kosa la kuchoma mifuko hiyo karibu na kiwanda hicho kilichopo maeneo ya wananchi wanaoishi, jambo ambalo ni kinyume na kanuni ya mazingira ya nambari 3 ya mwaka 2015.

Mshitakiwa huyo alikubali na kuiomba mahakama kumsamehe na atafata sheria zilizowekwa na serikali, ambapo mwendesha Mashtaka alisema upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama itoe adhabu.

Baada ya maelezo hayo,  Hakimu Mwanaidi alimtaka mshitakiwa kulipa faini ya shilingi 1, 000,000, ambapo kwa kosa la kwanza alitakiwa kulipa faini ya shilingi 400,000, la pili shilingi 150,000 na la tatu alitakiwa kulipa shilingi 400,000, na kosa la mwisho alitakiwa kulipa shilingi 50,000.