BERLIN, Ujerumani
MSHINDI wa nishani ya fedha katika Olimpiki za Rio 2016, Hyvin Kiyeng, amempiku bingwa wa dunia, Beatrice Chepkoech kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu.

Hiyo ni baada ya Kiyeng kuibuka malkia wa mbio za mita 3,000 kuruka vihunzi na maji kwenye kivumbi cha ISTAF Berlin, Ujerumani mbio zilizofanyika Jumapili iliyopita.

Wakenya hao walikuwa nyayo kwa nyayo hadi kihunzi cha mwisho. Hata hivyo, Kiyeng aliyeibuka bingwa wa dunia mnamo 2015, alimpigia hesabu Chepkoech katika hatua ya mwisho na kufika utepeni kwa muda bora wa dakika 9:06.04.

Kiyeng alimbwaga Chepkoech kwa mara ya mwisho mnamo 2017 walipotimua vumbi la michuano ya Doha Diamond League.
Miaka mitatu baadaye, mtimkaji huyo aliridhika na medali ya fedha katika mbio za World Athletics Tour zilizoandaliwa jijini Berlin, Ujerumani.(AFP).