WASHINGTON,MAREKANI

Watu kumi wameuawa kwenye matukio ya ufyatuaji risasi katika mji wa Chicago kwenye jimbo la Illinois nchini Marekani.

Watu wasiopungua 15 walipigwa risasi katika ghasia zilizojiri kwenye siku za mapumziko yanayohusiana na Siku ya Wafanyakazi nchini Marekani yaani tarehe 7 na 8 mwezi huu wa Septemba katika mji wa Chicago.

Watu kumi waliuliwa katika ufyatuaji risasi huo akiwemo mtoto mdogo wa miaka nane.

Maofisa wa maabara za jinai katika Chuo Kikuu cha Chicago walitangaza kuwa,mabarobaro 37 walio na umri chini ya miaka 18 na watoto sita wenye miaka chini ya kumi waliuliwa mwaka huu wa 2020 baada ya kufyatuliwa risasi huko Chicago.

Marekani hivi sasa inashuhudia wimbi la ghasia, vitendo vya uporaji  na mashambulizi ya kutumia silaha.

Vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha katika mji wa Chicago vina rikodi mbaya zaidi na mji huo ni moja ya miji inayoathiriwa pakubwa na ghasia na vitendo vya jinai nchini Marekani.

Kwa mwaka maelfu ya watu wanauliwa au kujeruhiwa kwa risasi katika maeneo mbalimbali nchini Marekani.

Hakuna Serikali yoyote ya Marekani iliyofanikiwa kuweka sheria ya kudhibiti umiliki wa silaha na zile zinazopasa kuuzwa kwa watu nchini humo kutokana na nguvu ya lobi za makampuni yanayouza silaha licha ya makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu nchini humo kutaka suala hilo lichukuliwe hatua madhubuti.