NA LAYLAT KHALFAN
HIVI karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imefanya mabadiliko ya sheria ya vileo sura ya 163 ya mwaka 1928 ili sheria mpya inayokwenda na wakati ianze kutumika.
Kwa mujibu wa sheria hiyo ni lazima kuundwa bodi ya usimamizi wa vileo itakayofuata sura 163 ya mwaka 1928 ambayo awali iliongoza usimamizi, uuzwaji vileo na kutunga sheria mpya ya namba 9 ya mwaka 2020.
Uwepo wa bodi hiyo ya kudhibiti vileo Zanzibar ni matakwa ya sheria hiyo ambayo itakuwa na wajumbe sita ikiongozwa na mwenyekiti kama ilivyoelekezwa chini ya kifungu cha 8 (1) sheria ya kudhibiti vileo ya namba 9 ya mwaka 2020.
Aidha, sheria hiyo ilikuwa inaongoza mpango mzima wa usimamizi, uuzwaji,usambazaji, uhifadhi, uagiziaji na mambo mengine yanayofanana na hayo kama inavyoelezwa katika kifungu cha 12 (1) a ya sheria hii.
Sheria iliyokuwaika awali ya mwaka 1928 ilikuwa imepitwa na wakati kwa kuwa likuwa inaruhusu kuwa na vilabu visivyozidi vitatu tu lakini kwasasa kutaruhusiwa kuwa na vilabu vingi ila vitakuwa na udhibiti mkubwa ili kuona kwamba havikiuki mila, silka na utamaduni wa wazanzibari.
Takwimu inaonyesha pombe nyingi inanywewa Zanzibar kuliko mikoa mengine ya Tanzania bara kutokana na sheria iliyokuwepo ilikua na udhibiti mdogo wa biashara hiyo.
Hali hiyo inasababishwa na uingiaji wa pombe nyingi za magendo zinazoingia Zanzibar hali ambayo husababisha watu kulewa mpaka kuvuka mipaka na kusababisha uhalifu na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na bidhaa hiyo.
Kwa kua bidhaa ya vileo inayoingia nchini pengine asilimia tano tu ndio inayolipiwa kodi iliyobaki yote hailipiwi hiii inatokana na kila mtu kupata uwezo wa kuagiza, sasa sheria hii inaweka masharti ya udhibiti kwa watu wote wakiwemo waagizaji ili kodi ya serikali ipatikane.
Kwa mnasaba huo utaratibu wa kanuni itakayokuwepo baadae itaeleza uwepo wa makampuni machache ambayo yatasajiliwa rasmi baada ya kupewa kibali na leseni na bodi hiyo.
Wakati umefika sasa kwa bodi hiyo kuzingatia sheria na kanuni pale wanapotekeleza majukumu yao ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa katika utekelezaji wa sheria hiyo.
Kwa kuwa kanuni tayari zimeshakamilika na zipo katika hatua ya kutangazwa katika gazeti rasmi la serikali ili kutekelezwa hivyo wahusika ni lazima wafanye kazi kwa mujibu wa sheria hiyo.
Iwapo wahusika watatimiza wajibu wao ni wazi kuwa, bodi itakuwa na meno hasa katika ukaguzi kwenye maeneo ya wauzaji, maghala ya kuhifadhia vileo kwa lengo la kuwafanya wamiliki wa maghala hayo kufuata tararibu zilizowekwa.
Sambamba na hilo lakini tunaamini kuwa yale mapato ya serikali yalikuwa awali hayapatikani sasa yatakuwa na udhibito mkubwa baada ya bodi hiyo kupewa meno.