NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kujenga mahakama maalum ya kusikiliza kesi za watoto ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja.

Ombi hilo lilitolewa na Kaimu Hakim dhamana wa Mahakama ya Mkoa wa Kusini Unguja, Said Hemed Khalfan, alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mwera.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuleta ufanisi katika usikilizaji wa kesi na kusaidia kupunguza mrundikano, kwani ili mtoto aweze kutoa ushahidi vizuri anahitaji utulivu, hivyo kuwepo kwa mahakama hiyo itakuwa chachu ya kufanikisha usikilizaji wa kesi hizo.

“Mahakama ya watoto inakuwa na mazingira maalum ambayo yanamuwezesha mtoto kutoa ushahidi kwa amani bila ya hofu, lakini mahakama hii  inasikiliza kesi mbalimbali na inamchanganyiko wa watu tofauti ikiwemo askari, haliambayo inawafanya baadhi ya watoto kuwa na woga na kusababisha mahakama hiyo kukosa ufanisi wa kusikiliza kesi hizo,”alisema.

Alifahamisha kwamba kutokana na changamoto hiyo hivisasa mahakama hiyo imeweka siku maalum kwa ajili ya kusikiliza kesi hizo, hivyo ni vyema serikali kuliangalia suala hilo kwa kulipatia ufumbuzi, ili kuwafanya watoto hao kuweza kupata haki zao.

Alisema kesi za watoto zinamazingira yake ya kusikilizwa hivyo haipaswi kuwa na mahakama iliyochanganyika na kesi nyengine, kwani kufanya hivyo kunawaweka katika wakati mgumu watoto hao.