NA ZAINAB ATUPAE

TIMU ya soka ya Valentina (KVZ) ya ligi kuu ya Zanzibar, imeendelea kutembeza kichapo katika mechi za kirafiki baada ya kuichapa mabao 3 – 2 timu ya Mchangani ya daraja la kwanza taifa kanda ya Unguja.

Huo ni mchezo wa tatu kwa KVZ ambapo wa kwanza ilikutana na timu ya Polisi na kuondoka na ushindi wa mabao 3 – 0, mchezo wa pili ilikutana na Mafunzo na kutoka na sare ya kufungana bao 1 – 1 na mchezo wa tatu ilicheza na timu ya Mchangani na kutoka na ushindi wa mabao 3-2.

Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Mao Zedong majira ya saa 10:00 jioni.Mechi hizo ambazo zina lengo la kujiandaa na mashindano ya ligi kuu ya Zanzibar pamoja na mashindano ya kimataifa.

Mabao ya KVZ yaliwekwa wavuni na Bashiru Khamis Daruweshi dakika ya 34 kwa njia ya penalti,huku bao la pili liliongezwa na Mohamed Massoud dakika ya 40 na kudumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.

Kurudi uwanjani kumalizia kipindi cha pili timu hizo zilingia kwa kasi kubwa,huku Mchangani kutafuta nafasi ya kurudi mabao na KVZ kuongeza mabao ili kuwa mshindi wa mchezo huo.

Lakini katika dakika ya 47 Omar Khamis wa timu ya Mchangani aliweka bao la kwanza, huku bao la pili liliongezwa na Said Khalid dakika ya 56.

Bao la jingine la timu ya KVZ liliongezwa na Mohamed Massoud dakika ya 78 na kudumu hadi mwisho wa mchezo huo.