TUCHUKUE fursa hii adhimu kuungana nanyi wasomaji wetu kwenye chapisho hili maalum, ambalo kimsingi tunaangazia miaka 10 ya uongozi wa awamu ya saba uliongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein.

Safari ya Dk. Shein kuiongoza Zanzibar ilianzia Juni 21 mwaka 2000 wakati alipofika katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui kuchukua fomu ya kuomba urais wa Zanzibar kuchukua nafasi ya Dk. Amani Abeid Karume.

Nyota njema ilionekana siku hiyo, kwani baada ya kuchukua fomu mkutnao wake wa kwanza na waandishi wa habari ulifantika pale hoteli ya Bwawani, ambapo alieleza kwanini ameamua kuchukua fomu.

Katika mkutano huo, Dk. Shein alieleza sababu kubwa tatu zilizomfanya kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar ya kwanza ni kwamba azma yake imetokana na imani ya wanachama, wapenzi wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar waliyonayo juu yake.

Aidha sababu ya pili aliitaja kuwa kutokana na imani hiyo ndiyo iliyompa moyo kwamba ataungwa mkono kwa dhati kwa lengo la kuijenga Zanzibar ili ipate maendeleo zaidi.

Kwenye mkutano huo, Dk. Shein pia alisema sifa za kugombea anazo hasa ikizingatiwa uwezo alionao, ari na ukerekwetwa katika suala zima la utumishi kwa nchi yake.

Mbali ya sababu hizo, kipaumbele chake chengine alichokitaja miaka 10 iliyopita ni kuhakikisha kuwa ana tatua changamoto za wananchi wa Zanzibar zikiwemo za umasikini, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii na kukuza maendeleo.

Hayo na mengine ndiyo aliyoyaahidi Dk. Shein miaka 10 iliyopita, ambapo kwa hakika kila eneo ambalo utamfanyia tathmini kiongozi huyo wa awamu ya saba ametekeleza vyema ahadi zake.

Wakati Dk. Shein akijiandaa kuondoka madarakani, kwa hakika wananchi wa Zanzibar tutakukumbuka kwa mengi sana ambayo umeboresha maisha ya wananchi bila ya kujali dini rangi, kabila ama mahali wanapotoka.

Hata hivyo, kubwa ambalo sisi tukiulizwa tutasema tunakukumbuka kwa kuifanikiwa kuitoa Zanzibar kwenye dimbwi la nchi masikini na kuifikisha kwenye uchumi wa kipato cha kati, hili ndio kiboko yao.

Aidha wananchi tutakukumbuka kwa uamuzi wako wa kuwaongezea mishahara wafanyakazi, tutakukumbuka kwa kuwapatia wazee pencheni tutakukumbuka kwa elimu bure, tukukumbuka kwa afya bure.

Kwenye upande wa afya hospitali kubwa umezijengea miundombinu ikiwemo kuvipatia vifaa tiba vya kisasa, huku dawa zikipatikana bila malipo yoyote. Kwenye elimu tumeshuhudia ongezeko la majengo ya skuli za ghorofa.

Aidha Dk. Shein wananchi tutakukumbuka kwa ujenzi wa miundombinu ikiwemo kutandika mtandao wa barabara visiwa vote vya Unguja na Pemba, sambamba na ujenzi wa madaraja ya kisasa.

Wananchi Dk. Shein watakukumbuka kwa kuviimarisha vyombo vya habari ikiwemo Shirika la Magazeti, ambapo tunathibitisha kwamba umetutendea haki, ziara zako ulizozifanya kwenye shirika hili tumekuwa dira na muongozo kwetu.

Kama tutahesabu kila kitu ulichofanya nafasi hii haitoshi, hivyo tumalizie kwa kuchukua fursa kukupongeza kwa dhati tunaamini umeitendea haki nafasi yako ya uongozi.

Hata hivyo, wakati unajiandaa kustaafu tunaomba geti la nyumba liwache wazi kwa wale wataokuja kwa kheri kwani kupata busara, baraka, na hakima zako tunaamini kwa uzoefu wako unaweza kuwa mshauri mzuri wa serikali ijayo.