LONDON, England
BAADA ya kuanza vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu ya England kwa kuitandika Brighton & Hove Albion magoli 3-0, meneja wa Chelsea, Frank Lampard, amekiri kufurahishwa na kiwango cha mlinda mlango wake, Kepa Arrizabalaga.

Lampard ameonyesha furaha dhidi ya mlinda mlango huyo raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 25, kufuatia maneno mengi yanayoelekezwa kwake kufuatia kuonesha kiwango kibovu.

Wachambuzi wa soka katika vyombo mbalimbali vya habari wamekuwa wakihoji nafasi ya kipa huyo kwenye kikosi cha Chelsea.

Mwishoni mwa msimu uliopita, Kepa alijikuta akimuachia Willy Caballero nafasi yake na yeye kusugua benchi.

Ni dhahiri mashabiki na wachambuzi wa soka walitarajia Chelsea wangelisajili kipa mwengine katika dirisha hili la usajili, mpaka sasa haijafanya hivyo.

Akizungumza baada ya mchezo wao wa kwanza wa EPL, Lampard amesema, “Ninafurahi kuwa na Kepa, kuhusu mkwaju ule, sidhani kama angefanya chochote cha ziada kuzuia asifungwe, lakini, nimeona ameongeza kiwango cha kujiamini. Kepa yupo hapa na ni kipa wetu.”

“Kama tutasajili mwengine itakuwa ni ushindani tu. Hiyo ni asili ya Chelsea, ni kwa timu nzima, tutaona itakavyokuwa.”