NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MWANZILISHI na mfadhili wa mashindano ya mpira wa miguu ya ‘Dande Cup’ Wilaya ya Wete Ahmed Seif Haji (Dande) amesema, ameanzisha mashindano hayo  kwa lengo la kukuza vipaji vya wanamichezo.

Alisema ni muda mrefu sasa Wilaya ya Wete imeanguka katika mchezo hasa mpira wa miguu, jambo ambalo lilikuwa likimhuzunisha, kwani kuna vijana wengi wana vipaji vinataka kuendelezwa.

Alisema  kupitia mashindano hayo anaamini watakuza vipaji vya wanamichezo hao na kuwa na viwango vya hali ya juu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mwanzilishi huyo alisema jumla ya timu 14 zitashiriki mashindano hayo.

Alieleza kuwa wachezaji wamepokea kwa furaha mashindano hayo, kwani kipindi cha nyuma walikuwa wanyonge kwa kukosa mashindano mbali mbali, huku wakisema kuwa vipaji vyao vilipotea.

Ali Mohamed Ali kutoka timu ya Kifumbikai Apari alisema kuanzishwa kwa mashindano hayo itakuwa heshima kwa yule atakaeibuka mshindi.

Aliwaomba waamuzi wawe na uaminifu pamoja na kuzingatia sheria, ili kuepuka migogoro isiyo lazima.