MONROVIA,LIBERIA

RAIS  wa Liberia Goerge Weah ametangaza kuwa,vitendo vya ubakaji ni tatizo la dharura la kushughulikiwa kitaifa na ametangaza sheria mpya za kupambana na mgogoro huo baada ya kesi za ubakaji kuongezeka nchini.

Sheria hizo mpya zilitangazwa baada ya maelfu ya raia wa Liberia kufanya maandamano ya kulaani kuongezeka vitendo vya ubakaji katika mji mkuu Monrovia.

Walifanya maandamano hayo kupaza sauti zao za kulaani ongezeko la ajabu la udhalilishaji huo wa kijinsia.

Rais Weah alisema atatangaza sheria mpya za kupambana na ubakaji na ataweka daftari la taifa la kuorodhesha vitendo hivyo.

Kiwango kikubwa cha ubakaji katika nchi hiyo mashakini kimezidi kuwaongezea matatizo wananchi ambao katika miaka ya hivi karibuni walikumbwa na janga kubwa la Ebola.

Katika ripoti yake mwaka 2016, Umoja wa Mataifa ulirikodi kesi 803 za ubakaji kwa kipindi cha mwaka mmoja katika nchi hiyo yenye wakaazi milioni nne na nusu.

Umoja huo ulitangaza kwamba uligundua,asilimia mbili ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia ndizo zilizotolewa hukumu mahakamani.

Vitendo vya ubakaji nchini Liberia ni vingi kutokana na miaka 14 ya vita vya ndani baina ya mwaka 1989 hadi 2003 ambapo katika miaka yote hiyo ya vita,vitendo hivyo vilikuwa jambo la kawaida, na sasa madhara yake yanazidi kujitokeza.