NA MWAJUMA JUMA

LIGI kuu ya Zanzibar ya soka la wanawake inatarajiwa kuanza rasmi leo katika viwanja vya Mao Zedong.

Ligi hiyo ambayo awali ilikuwa ianze Septemba 6, mwaka huu, lakini iliahirishwa kutokana na sababu mbali mbali.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo inaonesha kuwa leo kutakuwa na mchezo mmoja ambapo kwa mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya New Generation na Green Queens.

Ratiba hiyo itaendelea kesho uwanjani hapo saa 10:00 za jioni kati ya timu ya Women Fighter na Jumbi Queens.

Ligi kuu ya Zanzibar ya soka la wanawake inashirikisha timu tano ambapo timu mbili kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi na tatu kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Katibu wa kamati ya soka la wanawake Hawa Abdallah alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba, kwa kuanzia watakuwa na timu tano, ambapo mwakani wanatarajia kuongeza idadi ya timu kutoka skuli.

 Alisema tayari kamati yake imefanya juhudi ya kukutana na viongozi wa wizara ya Elimu kuwajuulisha juu ya uwepo wa timu za wanawake katika skuli ambazo zitakuwa zikishiriki ligi kila mwaka.