ZUHURA JUMA NA MARYAM SALUM, PEMBA
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad amesema endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi, atahakikisha anaimarisha maendeleo.
Akizungumza na wananchi wa chama hicho katika Uwanja wa Tibirinzi Chake Chake kwenye uzinduzi wa kampeni alisema moja ya kitu atakachokitekeleza ni ujenzi wa bandari.
Alisema kupitia bandari hiyo kutaruhusu makontena kuja moja kwa moja kisiwani Pemba, jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.
Alisema kuwa, ataifanya Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha biashara kwa kujenga bandari kubwa itakayosaidia kukuza uchumi na kipato kwa wananchi kitakachopelekea kupungua kwa umasikini.
“Nitajenga bandari kubwa na ya kisasa Unguja na Pemba, ili makontena yaje moja kwa moja kisiwani hapa, hii itasaidia vitu kuwa rahisi ambavyo watamudu kununua hata wananchi wa kipato cha chini”, alisema Maalim Seif.
Aliwaeleza wananchi kuwa, waakimpa ridhaa ya kuongoza atahakikisha kila mmoja anakuwa sawa mbele ya sheria, usalama wa raia na kulindwa.
“Mtakaponipa ridhaa nitahakikisha mnakuwa sawa mbele ya sheria na tutalinda haki za wananchi wote na mali zao”, alisema.
Aliwataka wananchi hao kwenda kwenye vituo vyao vya kupigia kura ifikapo Oktoba 28, kwani ni haki yao kikatiba na kisheria.
Aidha aliwaahidi wananchi kwamba endapo watampatia ridhaa ya kuwaongoza atahakikisha baada ya miaka mitano vijana wote wanapata ajira, ili waweze kujikimu kimaisha.
“Vijana wengi hawajaoa kutokana na uwezo wao kuwa ni mdogo, lakini mtakaponichagua, ndani ya miaka mitano nitawapatia ajira ili mjikwamue kiuchumi mpate kuwaowa akina dada ambao hawajaolewa”, alisema.
Aidha mgombea huo alisema, ataweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji, jambo ambalo litasaidia vijana kupata ajira na Taifa kupata maendeleo.