NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo Seif Shariif Hamadi amesema serikali ya awamu ya nane atakayoiongoza iwapo atachaguliwa itaimarisha sekta ya utalii ili kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Maalim Seif alieleza hayo wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Bububu Kwageji, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Alisema atahakikisha serikali inaweka miundombinu itakayochochea ongezeko la watalii wanaoingia nchini na kufikia watalii 800,000 kwa mwaka kutoka watalii 520,000 walioingia nchini mwaka 2019.

Alisema Zanzibar iko katika eneo zuri kitalii, hivyo kuna kila sababu ya kuongeza idadi ya watalii kwa kuongeza vivutio vya watalii.

Alisema katika kufanikisha hilo, Zanzibar itashiriki maonesho ya utalii katika nchi mbalimbali duniani pote kutangaza utalii na vivutio vilivyopo nchini.

Aidha alieleza kuwa atatafuta wawekezaji watakaoleta manufaa kwa wananchi wenye kipato cha chini ili nao wanufaike na raslimali zilizopo.

“Nitahakikisha vijana wetu wanapatiwa ajira, kunufaika na raslimali zetu na pale yatakapotokea majanga, wafanyakazi waendelee na kazi bila kupewa likizo za dharura,” alisema mgombea huyo.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho aliwahakikishia wakulima na wavuvi kuwa watanufaika na sekta ya utalii kwa kuwapatia mafunzo vijana ili wajiajiri na kushindana na vijana wengine kutoka nchi nyengine kwenye ajira zitokanazo na utalii.

Vile vile mgombea huyo alielezea kulinda silka na utamaduni wa Mzanzibari hasa suala la mavazi pale watalii wanapoingia katika jamii ili kulinda heshima ya Zanzibar.