NA BAKAR MUSSA, PEMBA

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad amesema kama atapewa ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, atahakikisha wakulima wa zao la karafuu na viungo wananufaika.

Maalim Seif aliyaeleza hayo katika kijiji cha Konde wilaya ya Micheweni ikiwa ni muendelezo wa kampeni kupitia chama hicho katika kisiwa cha Pemba.

Alisema kazi ya serikali yake itakuwa ni kukusanya kodi ndogo ili kuwafanya wakulima wapate faida kubwa na waendeleze kazi yao hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Alieleza kazi kubwa ya serikali yake ni kuwapatia mbinu na mazingira ya wakulima wa karafuu pamoja na bidhaa za viungo vyengine ili iwe ni njia ya kukuza uchumi Zanzibar.

“Tunataka kuwalea wakulima wetu wa bidhaa za viungo ili waweze kuitangaza Zanzibar katika masoko ya ulimwengu ili baadae wafanyabiashara za viungo waje Zanzibar kununua wenyewe”, alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema katika utawala wake atawashauri wakulima wa bidhaa za viungo kujikita zaidi kwenye bidhaa za viungo ambavyo vitaleta tija za haraka kwao na serikali kwa ujumla.

Mwenyekiti huyo wa ACT-Wazalendo alisema kazi nyengine ya kufanya ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mifugo bora na soko la uhakika.

Alieleza atahakikisha huduma zote za mifugo zinapatikana ili kile kinachozalishwa kina kuwa bora katika masoko yote.

“Tutahakikisha viwanda vya madawa na vyakula vya mifugo yote vinapatikana hapahapa kwetu ili iwe rahisi wafugaji kuwahudumia mifugo yao”, alieleza Maalim Seif.

Alisema wafugaji wengi wa kuku visiwani Zanzibar wameacha kufanya kazi hiyo kutokana na upatikanaji na ughali wa dawa na vyakula visiwani Zanzibar.

Akizungumza mbele ya mgombea huyo mfugaji wa kuku katika kijiji cha Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba, Humud Muhammed Said alisema kama ingalikuwa chakula cha kuku kinatengenezwa Zanzibar hata tija ingaliongezeka.