BANGKOK,THAILAND

MJI mkuu wa Thailand, Bangkok umekumbwa na maandamano makubwa ya kuipinga Serikali yaliyoendelea usiku kucha.

Waandamanaji wengi wao wakiwa ni vijana, wanatoa wito wa marekebisho ya katiba na mageuzi ya utawala wa kifalme.

Pia waliingia katika kampasi ya Chuo Kikuu cha Thammasat, wakipenya ulinzi wa polisi na kuushikilia uwanja uliopo nje ya Jumba Kuu la mfalme.

Waandaaji wa maandamano hayo walisema zaidi ya watu 50,000 wanashiriki.

Idadi hiyo inafanya maandamano hayo kuwa makubwa miongoni mwa yaliyowahi kufanyika wakati wa utawala huu wa Waziri Mkuu Prayut Chan-o-cha.

Prayut aliratibu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2014 na kuiongoza Serikali ya mpito,aliendelea kukaa madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Waandamanaji wanamshutumu kwa kuchukua msimamo wa kidikteta huku akiungwa mkono na jeshi. Pia wanaukosoa ufalme kwa kuunga mkono utawala huo.

Manifesto inayohusu mambo kumi ilisomwa kwenye maandamano hayo, ikitoa wito wa hitimisho la kikatiba linalokataza ukosoaji dhidi ya mfalme.

Mabadiliko ya utawala wa kifalme ni ajenda nyeti nchini humo, ambako shutuma dhidi ya ufalme ni kosa linaloweza kupelekea kifungo cha muda mrefu jela.

Lakini mwanasheria wa haki za binadamu anayetekeleza jukumu ongozi katika maandamano hayo alisema mabadiliko hayo yana thamani ya mtu kuwa tayari kuhatarisha uhuru wake.