NA KHAMISUU ABDALLAH

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimepinga kauli zinazotolewa na baadhi ya vyama vya siasa vinavyodai kwamba chama hicho kinashirikiana na dola katika kuhakikisha demokrasia haifuati mkondo wake.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdullah Juma Saadala (Mabodi) aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Kisiwandui mjini Zanzibar.

Alisema CCM haikupendezwa na tamko hilo ambalo linakwenda kinyume na chama hicho wakati wote katika kuhubiri amani ya nchi.  

Aidha alisema CCM haina siku iliyohubiri na kulaumu serikali na kusifia serikali za nje, kusifia wananchi na kubeza amani ya nchi lakini vipo vyama vimeanza kuzungumza lugha ambazo hazina maslahi mapana na nchi ya Tanzania.  

“Mimi nikiwa kama mkurugenzi wa uchaguzi ndani ya CCM kwa Zanzibar napinga vikali kauli hizi zinazotolewa na ndugu zetu, sisi tulijitahidi kukaa kimya ili kuelezea na kuamini kwamba amani na mshikamano tulionao ndani ya Zanzibar ndio nyenzo pekee itayotupeleka mbele ndani ya uchaguzi,” alisema.

Mabodi alisema imefika wakati kwa wananchi wa Zanzibar kuwa macho na kuwa watulivu katika kushiriki kampeni kwa kusikiliza sera njema na sio vituko vinavyotolewa na baadhi ya vyama ambavyo vinataka kuiharibu amani iliyopo.

Naibu Mabodi, alivisisitiza vyama vinavyoingia kwenye kampeni kuacha mara moja kuzungumza taarifa ambazo zinabeza vyama vyengine, usalama wa nchi na kubeza amani ya nchi iliyopo inayosimamiwa na vyombo vya dola.

Alisema, CCM inaamini kwamba nchi na dola itashirikisha na kuisimamia amani ya nchi na kueleza sera zao katika kampeni zinazotarajiwa kuanza Septemba 12 mwaka huu mpaka kwenye ushindi.

Akizungumzia kuweka pingamizi kwa wagombea Naibu Mabodi alisema CCM imetimiza matakwa ya sheria katika uchaguzi wa mwaka huu katika kuweka pingamizi kwa wagombea.

Alisema isiwe kituko kwa CCM kuweka pingamizi kwa maeneo ambayo wapo watu ambao wanasema ni kwao bila ya kujali kuwa nchi ni ya watu wote.

“Wapo watu wamekosea majina yao, hawajui kusoma mtu huyu amekosea kujaza fomu una uhakika gani kwamba amejaza fomu kwa kudanganya apite tu halafu awabeze wananchi tumeweka pingamizi na tumefanikiwa sana kwa upande wa ubunge lazima haki itendeke,” alisisitiza.