ABUJA,NIGERIA

MADAKTARI  wakaazi nchini Nigeria wameanza mgomo wao wa pili kwa mwaka huu wakilalamikia mazingira mabaya ya kazi pamoja na marimbikizo ya malipo yao wakati huu wa kuenea virusi vya Corona.

Mgomo huo ulioanza Jumatatu iliyopita unaendelea na uliathiri pakubwa sekta ya afya nchini Nigeria hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Abuja inafanya juhudi za kukabiliana na ueneaji wa virusi vya Corona.

Madaktari wakaazi ni wahitimu wa skuli za udaktari ambao wanapata mafunzo kwa ajili ya kubobea katika taaluma maalumu ya udaktari.

Dakta Aliyu Sokomba, Mkuu wa Muungano wa Madaktari Wakaazi nchini Nigeria alisema kuwa, mgomo huo unajumuisha madaktari wakaazi 16,000 katia ya madaktari wote 42,000.

Aidha alisema kuwa, mgomo huo utaendelea mpaka pale madai yao yatakaposikilizwa na kupatiwa ufumbuzi na kwamba, madaktari wote wa vituo vya Covid-19 walijiunga na mgomo huo.

Mwezi Juni mwaka huu, Madaktari hao walifanya mgomo pia wakidai kuboreshwa mazingira yao ya kazi kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona.

Mbali na kuboreshwa mazingira ya kazi, madaktari hao wanataka kupatiwa bima ya maisha na posho ya ziada.

Chris Ngige, Waziri wa Kazi na Ajira  wa Nigeria aliwataka madaktari hao kusitisha mara moja mgomo wao na kurejea kazini.

Hadi sasa Nigeria ilisajili kesi 55,456 za maambukizo ya Corona huku watu 1,067 wakiwa wamefariki dunia nchini humo kwa maradhi ya Covid-19.

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari ilikuwa ikikosolewa kutokana na kushindwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo hasa ukosefu wa usalama, kudorora uchumi na vitendea kazi duni katika sekta ya afya.