KHARTOUM, SUDAN

OFISI ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa zaidi ya watu nusu milioni wa Sudan wameathiriwa na mafuriko makubwa yanayoikumba nchi hiyo kutokana na mvua kali zilizosababisha kujaa maji ya Mto Nile.

Taarifa iliyotolewa na OCHA ilisema kuwa, hadi Jumanne iliyopita zaidi ya watu 557,000 walikuwa wameathirika na mafuriko nchini Sudan na kwamba maeneo ya Khartoum, kaskazini mwa Darfur na Sinar ndiyo yaliyopata hasara kubwa zaidi kutokana na mafuriko hayo.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa iliongeza kuwa zaidi ya nyumba 111, 000 zimesombwa na mafuriko ya sasa nchini Sudan.

OCHA ilitangazarisha kuwa mvua kali zinazoendelea kunyesha nchini Sudan zinatishia kuzusha maradhi ya kuambukiza na kukwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi  ya virusi vya corona huku watu wasiopungua 103 wakifariki katika mafuriko ya Sudan na wengine 56 wamejeruhiwa.

Tarehe 5 mwezi huu Baraza la Usalama wa Taifa la Sudan lilitangaza hali ya hatari kote nchini humo kutokana na mafuriko makubwa yanayoikumba nchi hiyo. Sudan pia iliomba msaada wa jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathiriwa na mafuriko nchini humo.