ADDIS ABABA,ETHIOPIA

WAZIRI  wa amani wa Ethiopia Muferiat Kamil, amesema watu karibu 217,000 wamepoteza makaazi yao kutokana na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika miaka 30 iliyopita nchini Ethiopia.

Kamil alisema katika maeneo kadhaa mafuriko hayo yalikuwa makubwa kabisa katika karne moja iliyopita na yalisababisha watu 217,000 kupoteza makaazi yao na wengine 363,000 kuathiriwa vibaya.

Majimbo matano yaliyoathiriwa vibaya na mafuriko hayo ni Gambella, Kusini,Afar, Oromia na Amhara.

Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema kuwa watu milioni 15.1 nchini Ethiopia wanahitaji msaada wa chakula kutokana na athari za mafuriko,janga la COVID-19, nzige wa jangwani na maafa mengine yanayosababishwa na binadamu.

OCHA inasema inahitaji dola za kimarekani bilioni 1.44 kukidhi mahitaji ya kibinadamu nchini Ethiopia,lakini mpaka sasa bado haijapata fedha za kutosha kuendeleza operesheni zake.