NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya mwanzo Mwanakwerekwe imeiahirisha kesi inayomkabili mshitakiwa Sadam Hussein Tajo (20) mkaazi wa Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja hadi Septemba 16 mwaka huu.

Hakimu Omar Said wa mahakama hiyo aliiahirisha kesi hiyo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi dhidi ya kesi inayomkabili mshitakiwa huyo mahakamani hapo na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu 326 (1) cha sheria ya makosa ya jinai namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kuwa kwa makusudi na bila ya halali aliviharibu vyarahani saba mali ya Hassan Tajo Tafuta vikiwa na thamani ya shilingi 400000 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Koplo Vuai alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 9 mwaka jana saa 10:40 jioni huko Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Mshitakiwa huyo yupo nje baada ya kukamilisha masharti ya dhamana baada ya kuwasilisha wadhamini wawili waliotoka kwenye familia ambao kila mmoja alimdhamini kwa shilingi 1,000,000 za maandishi pamoja na kuwasilisha kopi zao za kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua ya Sheha na yeye mwenyewe kujidhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi.