WAPENZI wasomaji wa Zanzibar Leo, kwa makusudi nimewatayarishia upishi mwanana wa Mahshiy Kusa -Mamumunya Yaliyojazwa.

Pishi hili kwa kawaida hutumiwa nchi za Shaam, lakini hata hapa Zanzibar watu wanaweza kubadilisha chakula na kujaribu kupika siku moja moja.

Hivyo basi leo nitawafahamisha namna ya kutayarisha vipimo, mahitaji na namna ya kuyasarifu masaptasapta haya, Karibuni tuungane katika pishi hili.

VIPIMO 

Mamung’unye  ndogo ndogo (Kusa) – 1 Kilo

Nyama ya kusaga –  ½ kilo

Tangawizi iliyosagwa -1 kijiko cha chai

Mchele wa Kimisri (Egyptian rice) -1 kikombe

Kitunguu maji (chopped au kilichosagwa) – 1

Garam masala ya unga – ½ kijiko cha chai

Tomato paste  – 1 kibati

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 3 chembe

Mafuta ya zaytuni – 3 Vijiko vya supu

Pilipili manga ya unga  -1 kijiko cha chai

Chumvi    –  kiasi

Maggi  (cubes) vidonge vya supu –  2 

Baqduni (parsley) na kotmiri iliyokatwa ndogo ndogo  – ½ kikombe

Maji –  2 Vikombe

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kaanga vitunguu katika kwa mafuta moto mdogo mdogo hadi vigeuke viwe laini au vibadilike rangi ya brauni iliyo khafifu.

Tia nyama, thomu na tangawizi, garam masala, pilipili manga, chumvi  na endelea kukaanga ipikike.

Tia mchele na uchanganye vizuri.

Zikwangue (toa nyama ya ndani) kusa ziwe na shimo, osha na weka tayari kwa kujazwa.

Jaza  na mchanganyiko huo wa nyama na mchele katika kusa.

Panga vipande vya viazi chini katika sufuria na upange juu yake Kusa.

Katika bakuli, changanya nyanya ya kopo na maji ya moto kidogo, thomu iliyosagwa, mafuta ya zaituni, pilipili manga, chumvi, chambua vidonge vya Maggi, tia baqdunis na kotmiri na uchanganye vizuri.

Mimina sosi hiyo juu ya kusa, funika vizuri kwa kuwekea kitu kizito juu yake na pika moto wa kiasi kwa muda wa saa.

Epua, funua itoke mvuke, pakua kusa katika sahani na pambia viazi juu yake, ikiwa tayari kuliwa.