Mwashungi Tahir       

Vijana vijana vijana ni nguvu kazi ambayo inasimama imara kujenga Taifa ambalo Taifa husika linawatizama vijana kama vijana  katika Nchi yao kwani ndio rasilimali kubwa katika kuchapuza maendeleo.

Kwa kuwa vijana ndio nguzo katika mustakabali mzima wa kuimarisha  maendeleo , kutoa hamasa kwa wenzao na pia kuwa mstari wa mbele kwenye mambo yote .

Tunashuhudia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dkt Ali Mohammed Shein, jinsi inavyowapa kipaumbele katika kuwaimarisha vijana ili waweze kuwa nguzo imara katika nchi yao kwa kuweza kuyasimamia mambo mbali mbali ya maendeleo .

Serikali imesema itaendelea kuwaunga mkono vijana Kutokana na  jitihada zilizochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk, Ali Mohamed Shein ili kufanikisha malengo yao katika kuleta maendeleo katika Taifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amesema wakati wa kulivunja Baraza la Tisa la Wawakilishi bado tatizo la ajira kwa vijana lipo na Serikali inaendelea kuchukua hatua kwanza kuwaandalia vijana mafunzo ya amali  katika vituo vya Serikali, katika vituo vya Amali na katika kituo cha Ukuzaji Wajasiriamali huko Mbweni.

Pili vijana wamepatiwa mikopo, kwa lengo la kujiajiri wenyewe kwenye shughuli zao , Tatu wamewezeshwa kwenye kilimo kama vilem pilipili hoho ufugaji na ushoni na pia zaidi ya vijana 39,499 wamepatiwa mikopo yenye thamani ya TZS Billioni 4.32 kwa ajili ya kuwaendeleza  katika kilimo, ufugaji na ushoni.  

Hivi karibuni katika maandalizi ya kuingia katika mchakato wa uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2020 tumeona chaguzi za jumuiya za chama  zimefanyika ikiwemo UWT, WAZAZI na VIJANA  na kupatikana viongozi  waliochaguliwa kwa ridhaa za wanachama kwa kuwaona wanafaa katika kupeperusha bendera kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi na kuingia ndani ya Baraza la Wawakilishi na Bunge kwa nia ya kutoa maamuzi yanayofaa.

Mwandishi wa Makala haya anamuelezea mmoja ya waliobahatika kuingia Baraza la Wawakilishi kupitia Umoja wa Vijana wa CCM ni Hudhaima Mbaraka Tahir ambae ameibuka mshindi wa pili kati ya watu saba  waligombea nafasi hiyo  kuungana na mshindi wa kwanza kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi katika chombo hicho cha kutunga sheria Zanzibar.

Hudhaima Mbaraka Tahir alizaliwa tarehe 15.4.1995 katika mtaa wa Rahaleo, Mkoa wa Mjini Magharibi akiwa ni mtoto wa pili katika familia yake. Alianza elimu ya msingi katika Skuli ya Rahaleo  mwaka 2003 hadi 2009 baadae alijiunga na elimu ya Sekondari Darajani mwaka 2010 hadi 2013.

Katika mwaka 2014 Hudhaima alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma (IPA) akiwa mwanafunzi wa cheti katika fani ya Uhusiano ya Umma na alijiunga na mafunzo ya Diploma ya Mawasiliano ya Umma (Mass Communication) mwaka 2015 hadi 2017 katika chuo hicho hicho.

Mwaka uliopita, 2019 Hudhaima Mbaraka Tahir alianza masomo ya Shahada ya kwanza ya Mass Communication katika Chuo cha Kampala University iliopo Uganda.

Safari yake iliendelea  ya kuhudumia Jamii ilianza mwaka 2008 kwa kujiunga na Baraza la watoto katika Shehia ya Rahaleo kwa lengo la kupigania haki na wajibu wa mtoto mwaka 2010 – 2012 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Tanzania.

Aliingia rasmi katika shughuli za siasa kwa kujiuga na Jumuiya ya Umoja wa Vijana katika tawi lake la Rahaleo mwaka 2012 na alichaguliwa kuwa Katibu wa Vijana Tawi wa tawi hilo.

Kutokana na juhudi kubwa ya kuimarisha Jumuiya ya Vijana ndani ya Tawi lake, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini mwaka 2017 na alikuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji nafasi ambayo anaendelea nayo hadi hivi sasa katika Wilaya ya Mjini.

Huzaima Mbaraka alipata nafasi ya kwenda Burundi kujifunza ulinzi wa mtoto mwaka 2009 na alipata fursa ya kuiwakilisha UVCCM katika mkutano wa Vijana wa Bara la Asia uliofanyika nchini China mwaka 2019.

Katika harakati za kushirikiana  na vijana wenzake na kuhakikisha anatoa mchango wake, mwaka 2016 alikuwa Naibu  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO).  

Mwashungi Tahir

Akizungumzia azma yake ya kuingia katika mchakato wa kuwania nafasi ya  uwakilishi ni kutaka kupigania, kuwatetea na kuwaunga mkono vijana wenzangu katika masuala ya elimu na mambo mengine wanayokabiliana nayo.

‘’Nimeamua kuchukua nafasi hii ya viti maalumu kupitia vijana kuingia katika Baraza la Wawakilishi kwa kupigania maslahi ya vijana wenzangu katika mambo mbali mbali ya maendeleo ndani ya Mkoa wa Mjini,” alisema Hudhaima.

Alisisitiza kuwa atakapoingia katika chombo hicho cha kutunga sheria atachukua  uthubutu wa kupaza sauti kuhakikisha vitendo vya udhalilishaji ambavyo kwa sasa vimeshamiri ndani ya Mkoa wa Mjini vinapungua na hatimae vinaondoka kabisa.

 Aliwataka vijana wenzake kuchukia kwa nguvu zao zote na kuunga mkono juhudi za Serikali zinazoendelea kuchukuliwa katika katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinaleta aibu kwa Taifa.

Akizungumzia suala la ajira ambalo limekuwa tatizo sugu kwa vijana wengi, atahakikisha fedha za ruzuku ya vijana inayotolewa na Manispaa zinawasaidia kuwaletea maendeleo kwa kuwajengea masoko  ili waweza kujiajiri.

Kuhusu tatizo la madawa ya kulevya linaloathiri vijana, ambao ni nguvu kazi  ya Taifa, aliahidi atahakikisha vijana wanakusanywa na kupewa elimu juu ya athari kutumia madawa hayo na mbinu za kuachana nayo na kuwaandalia mipango ya kiuchumi ili waweze kujishughulisha na kukosa muda wa kukaa vijiweni.

Nawaomba vijana kujenga  mashirikiano ya pamoja katika kupanga mipango ya kujiletea maendeleo ndani ya Mkoa wa Mjini na tulete mabadiliko makubwa.

“Vijana wenzangu naomba ushiriki wenu kwangu ili nipate wepesi wa kufanya kazi  na nyie na kuweza kupata maendeleo ndani ya Mkoa wetu kwa pamoja tunaweza,” alisema Hudhaima.

Matarajio yangu ni kuona vijana wenzangu tunakaa pamoja tunashauriana kwa mambo yatakayonyanyua katika kupeleka mbele gurudumu la maendeleo na mafanikio makubwa ndani ya Mkoa huo.

Tumeona jinsi Serikali inavyowapa kipaumbele vijana kwa kuweka siku maalum kila ifikapo tarehe 12 August duniani kote huadhimisha    kwa lengo la kuwaweka pamoja ambapo ujumbe wa mwaka huu 2020  ni KIJANA SHIRIKI UCHAGUZI DUMISHA AMANI.