NA ABOUD MAHMOUD

KLABU ya soka ya Malindi inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar imeanza mchujo wa kuchagua wachezaji ambao wanatarajia kuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.

Mchujo huo umeanza jana na utachukua siku tano ambapo mara baada ya hapo ndio uongozi wa klabu hiyo, pamoja na kocha wataweka bayana wachezaji wangapi waliowachukua na kuwaacha.

Akizungumza na Zanzibar Leo kocha mkuu wa klabu hiyo, Mohammed Badru alisema lengo la kufanya hivyo ni kupata wachezaji imara na wenye viwango, ambao watasaidia kuiweka timu katika nafasi nzuri msimu ujao.

“Tumeona kwanza bora tuanze na mchujo utakaochukua siku tano haya ndio maamuzi mazuri ya kuchagua wachezaji gani tuwachukua na wepi tuwaache kwa ajili ya malengo tuliojipangia katika timu yetu,”alisema.

Kocha huyo alisema mara baada ya kumaliza kwa mchujo huo  klabu itatangaza rasmi wachezaji waliowasajili ndani ya kikosi hicho.

 “Bado kutaja kikosi kwa sababu hatujachagua tukishapata wachezaji ambao tunawataka tutasema na mashabiki na  wanachama pamoja na wapenda soka wote wanatajua lakini kwa hivi sasa bado kuzungumzia hilo,”alisema.