NA MWANAJUMA MMANGA

KLABU Ya Malindi SC imesema inatahakikisha inafanya vyema katika michezo yake ya ligi kuu Zanzibar msimu wa mwaka 2020/2021.

Hayo yameelezwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mohammed Badru Juma wakati akizungumza na gazeti hili katika uwanja wa Malindi baada ya kumaliza mazoezi.

Alisema ili kufikia malengo hayo atahakikisha anawaandaa wachezaji wake katika hali ya ushindani huku akiendelea kurekebisha makosa.

“Nina malengo mengi na pia nimekuja kuibadilisha timu najua kuna kazi kubwa,lakini kwa nguvu za Mungu hakuna kinachoshindikana”alisema.

Aidha alisema kuwa hivi sasa anaendelea kucheza mechi za kirafiki zinazolengo la kufanya mchujo wa kutafuta wachezaji ambao watawasajili.

Alisema tayari wameanza kucheza mechi na timu ya Mchangani inayoshiriki ligi daraja la kwanza na kutoka sare ya kufungana bao 1 – 1.

Alisema katika mechi hiyo ameona makosa mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.

 Aidha alisema katika mazoezi yake na mechi aliyocheza tayari ameona   wachezaji wanne ambao ataanza kuwasajili katika timu hiyo.

“Wachezaji wanne nimewaona lakini siwezi kuwataja kwa sasa, nitawataja baada ya kukamilisha usajili,” alisema.

Hivyo aliwahakikishia mashabiki na wapenzi wa timu hiyo msimu huu anarejesha hamasa na heshma ya klabu hiyo, kwa kufanya vizuri katika ligi.