NA KHAMISUU ABDALLAH

MKE wa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Maryam Mwinyi amewataka watoto wa kike kujitambua kwa kufuata mila silka na tamaduni zao.

Mama Maryam, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa skuli ya wanawake Benbella, ambapo aliwataka wasichana kuhakikisha wanajijengea misingi ya heshima na tabia njema.

Alisema mtoto wa kike ni nguzo muhimu katika jamii na maendeleo kwa ujumla, hata hivyo kitu cha kwanza ni muhimu kujijua na kuijua thamani yao.

Aidha alisema mara nyingi watoto wa kike wamekuwa wakiiga tamaduni za nje kupitia mitandao ya kijamii na kupoteza muelekeo wa kuzifikia ndoto zao za maisha ya baadae.

“Nawanasihi sana wanangu mjitambue kuwa watoto wema, kama watoto wa kike msiige tamaduni za kigeni sio mila zetu, tufuateni misingi ya dini yetu kwa kutengeneza jamii iliyo bora”, aliwaasa.

Aliwataka wanafunzi katika skuli hiyo kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha na msingi mkuu wa maendeleo, hivyo ni vyema wakajitahidi.

“Msikubali kudanganyika kuweni na ndoto na matarajio katika maisha yenu ya baadae taifa linahitaji viongozi mkiwemo nyinyi vitu vyengine vipo jielekezeni kwenye masomo huo ndio wajibu wenu kwa sasa kwani mshika mbili moja humponyoka,” aliwasisitiza.

Mbali na hayo, aliwasisitiza wanafunzi kupenda masomo ya sayansi kwani dunia ya sasa inakwenda kwa sayansi na teknolojia.

Kwa upande wake waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema lengo la serikali kuanzisha madarasa maalum ya wanawake ni ufaulu na idadi kubwa ya wanawake ukilinganisha na wanaume.

Alisema serikali inajitahidi kufanya mambo mengi katika sekta ya elimu, lakini changamoto za elimu kila siku zinakuwepo kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi mwaka hadi mwaka hasa watoto wa kike kuwa na muamko wa kusoma.

Alimpongeza kwa hatua yake ya kukubali kuwatembelea wanafunzi wa kike na kuamini kwamba ataikamata mkono na kuwa mlezi katika elimu ambayo ndio kila kitu katika taifa lolote duniani.

Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Zainab Mbwana Mgunda, aliipongeza serikali ya awamu ya saba chini ya Rais wa Zanzibar katika kutatua changamoto mbalimbali katika skuli hiyo ikiwemo vikalio.

Nao wanafunzi wa skuli hiyo walisema skuli yao inakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa upungufu wa vitabu na madarasa hasa kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ambayo inashusha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na kutosoma kwa wakati.