HAKUNA kero kubwa kwa sasa inayoikosesha raha sehemu kubwa ya jamii na kuzungumzwa kila kona wakati mwengine kwa hisia kali na wananchi wa Zanzibar ni ile inayoitwa ‘migogoro ya ardhi’.

Tunavyoamini wapo baadhi ya watu sio kwa bahati mbaya, bali kwa kukosa uzalendo na kuvutiwa na maslahi binafsi wamekuwa wakiitengeneza kwa makusudi hiyo inayoitwa ‘migogoro ya ardhi’.

Tatizo hili lipo kwa muda mrefu sasa, lakini katika kipindi cha miongo kama mitatu hivi pamoja na jitihada kadhaa kuchukuliwa na serikali, migogoro ya ardhi inazidi kukua badala ya kupungua.

Bila shaka zipo sababu kadhaa zinachangia ongezeko la migogoro ya ardhi, ikiwemo ile ya ongezeko la thamani ya ardhi yenyewe na ongezeko watu, ambalo linalazimisha mahitaji ya rasilimali ardhi nayo kuongezeka.

Katika hili, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa vizazi vijavyo, kwa sababu watu wanaongezeka kila uchao, lakini ardhi ya Zanzibar haiongezeki badala yake inazidi kupungua kwa kumezwa na maji ya bahari kama vile tunavyoishuhudia.

Ushahidi wa ardhi ya Zanzibar kumezwa na bahari hauhitaji vipimo vya kisayansi, kwani ukipata bahati ya kuvitembelea vijiji vilivyo kando kando bahari, wazee watakupa baadhi ya maeneo ambayo zamani shughuli za kijamii zilikuwa zikifanyika lakini sasa hivi maji ya bahari yamejaa.

Sababu nyengine kubwa inayochochea kujitokeza kwa migogoro ya ardhi kila uchao hapa Zanzibar ni zile za kiuchumi, hasa uwekezaji wa miradi kwenye sekta ya utalii.

Katika eneo hili kuna mvurugano mkubwa unaosababisha kuwepo kwa maslahi binafasi yanayosababisha malalamiko kadhaa, huku pia baadhi watendaji na viongozi kati ngazi za shehia, wilaya na mikoa wakihusishwa.

Kwa hakika ukiukwaji wa sheria tena kwa makusudi ndio kimekuwa chanzo kubwa cha migogoro ya ardhi kwenye sekta ya uwekezaji, tumekuwa tunajiuliza hawa wengine wasio na mamlaka ya ardhi, wanapata wapi mamlaka za udadali wa kuuza ardhi?

Suala la ukiukwaji wa sheria za ardhi pia limeelezwa bayana na vongozi wakuu wa Zanzibar akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Chakushagaza wanaojitia udalali wa ardhi ambao wengi wao ni matapeli wakiwemo baadhi ya viongozi hawakomi kwani wanaendelea na vitendo vyao hivyo pamoja na kuonywa na kukatazwa sana.

Inasikitsha baadhi ya masheha na madiwani katika baadhi ya maeneo nao wamejiingiza kwenye mchezo huo, huku tukijiuliza uwezo wa kuwa mdalali wa ardhi wameupata wapi na kwa mamlaka ipi wakati ardhi ya Zanzibar wote ni mali ya serikali.

Lakini tunawauliza kama suala limeshakatazwa na Rais na Makamu kwenye mikutano mbalimbali hivi viongozi hao wanataka aje nani tena awaeleze kuwa wanachokifanya sio halali?

Tunaeleza hivyo kwasababu hatuamini kama Mwenyezi Mungu anaweza kuleta mtume mwengine ama kushusha malaika kuja kutukataza uunjwaji wa sheria za ardhi.

Tunaziomba sana mamlaka lazima zihakikishe maofisa na viongozi wanaojihusisha na utapeli wa ardhi washughulikiwe kwa kupewa adhabu kali bila ya hivyo matatizo haya hayatamalizika.