KWA mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), zinaonesha kwamba hadi mwaka huu wa 2020 kuna wakimbizi takribani milioni 80.

Wakimbizi hao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamelazimika kuishi kama wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa.

Aidha takwimu za shirika hilo zimeeleza kuwa kuna watoto milioni 13 ambao wamelazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji kwenye maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Ongezeko la wakimbizi duniani linatokana na ukweli kwamba, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa ama kupuuza kudhibiti vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii.

Uganda ni moja ya nchi zenye kuhifadhi wakimbizi wengi, ambapo kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi nchi hiyo ina jumla ya wakimbizi milioni 1.4, ambapo asilimia 74 wanatoka nchini Sudan Kusini na waliobakia wanatoka nchini DRC.

Lakini kiukweli wakimbizi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo udhalilishaji, ambapo nchini Uganda zipo tuhuma kwamba wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanahusika kwenye udhalilishaji wa kingono.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakiwalazimisha wanawake wakimbizi kufanya nao ngono kwa kubadilishana na chakula.

Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai hayo ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya baadhi ya maofisa waoke huko katika eneo la kaskazini mashariki la Karamoja.

Uchunguzi huo wa kamati maalum ya Umoja wa Mataifa ulioanza mapema mwezi huu unafuatia madai ya manyanyaso ya kingono na dhuluma dhidi ya mwanamke na mfanyakazi wa shirika hilo katika eneo la Karamoja.

Inadaiwa kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakiwalazimisha wanawake kufanya nao tendo la ngono kwa kubadilishana na chakula.

Aidha yapo malalamiko kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa pia wanadaiwa kuingiza wanawake katika kambi ya umoja huo kwa ngono ya kulipwa katika wilaya ya Moroto.

Wafanyakazi hao wanaishi kwenye kambi ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) katika sehemu ya Karamoja ambayo zaidi ya watu 500,000 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

“Tumearifiwa kuhusu madai dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaoishi katika kambi ya WFP mjini Moroto. Tunachunguza madai hayo” alisema Amanda Lawrence Brown, msemaji wa WFP akiwa Nairobi, Kenya.

Brown aliongezea kusema kwamba hakuna mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, au mtu yeyote anayeishi katika kambi ya WFP anaruhusiwa kujihusisha katika unyanyasaji wa kingono au wa aina yoyote ile dhidi ya watu katika sehemu wanafanya kazi zao.

Hata hivyo, alikataa kusema idadi ya wafanyakazi wanaoishi kwenye kambi ya Moroto kutokana na sababu za kiusalama.

Alisema kwamba uchunguzi pia unafanyika kuhusu ripoti za kuvunjwa kwa kanuni za kiusalama na kwamba walinzi wanastahili kuwachunguza wageni wote wanaoingia katika kambi hiyo.

Mratibu mkuu wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Uganda, Rosa Malango, alisema kwamba alichukua hatua za kutaka uchunguzi kamili kufanyika kuhusiana na suala hilo.

“Natarajia kupata majibu kutoka kwa wakuu wa umoja wa mataifa ikiwemo kuwasimamisha kazi kwa mda maofisa waliohusika wakati uchunguzi unapoendelea”, aliandika Malango katika ujumbe wa barua pepe kwa viongozi wa juu wa umoja wa mataifa.

Malango alisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa haukubali kabisa unyanyasaji wa kingono na kwamba swala hilo linachunguzwa vipasavyo.

Inaripotiwa kwamba kundi la maofisa wa umoja wa mataifa walikosoa sana barua pepe aliyoandika Malango iliyofananisha Uganda na Haiti kutokana na madai hayo ya unyanyasaji wa kingono.

Kundi hilo limesema kwamba barua pepe ya Malago ina habari ambazo ni za siri sana na asingetuma kwa makundi ya ndani ya wafanyakazi wa umoja wa mataifa.

Kwa kusema kwamba Uganda ilikuwa inakaribia kufanana na Haiti, Malago alizingatia sakata ya shirika la Oxfarm ya kufunika ukweli kuhusu madai ya wafanyakazi wa shirika hilo la Uingereza kuwanyanyasa kingono waathiriwa wa tetemeko baya la ardhi la mwaka 2010, waliotegemea msaada wa chakula kutoka kwa shirika hilo.

Malago hata hivyo alisema kwamba barua yake kwa shirika la umoja wa mataifa, singetumwa kwa watu ambao hawafanyi kazi katika umoja wa mataifa.

Hii ni mara ya pili Umoja wa Mataifa kujikuta katika sakata inayohusisha eneo la Karamoja, itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2019, watu wanne waliugua baada ya kukula chakula kilichokuwa kimetolewa kama msaada na shirika la chakula duniani WFP na shirika hilo likashutumiwa kwa uzembe.

Eneo hilo lililo mpakani na Kenya, linakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kiangazi cha kila mwakam hivyo wakimbizi wengu hulazimika kutegema chakula kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.