MOSCOW,URUSI

URUSI imetoa lalamiko kali kwa Ujerumani kuhusiana na madai ya kupewa sumu kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, ikishutumu kuwa ni madai yasiyo na msingi na kuonya kuhusu hatari kubwa katika mahusiano ya kidiplomasia.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi ilimuita balozi wa Ujerumani nchini humo Geza Andreas von Geyr na kulalamika kuhusiana na shutuma hizo ilizosema hazina msingi pamoja na kutoa muda wa mwisho wa Urusi na kuitumia hali ya Navalny kama sababu ya kuidhalilisha nchi hiyo.

Urusi iliiomba tena Ujerumani kujibu ombi kutoka kwa mwendesha mashitaka wa Urusi kuhusu ushahidi,ikiwa ni pamoja na data za kitabibu, ambazo ziliifanya Ujerumani kutangaza kuwa Navalny, mmoja kati ya wakosoaji wakubwa wa rais Vladimir Putin, kuwa alipewa sumu inayoathiri mishipa ya fahamu ya Novichok.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo alisema kuwa kuna nafasi kubwa kwamba kinachotiliwa shaka kuwa ni kupewa sumu kwa Navalny kuliamuriwa na maofisa waandamizi wa Urusi.

Pompeo alisema Marekani inatathmini vipi inaweza kujibu hali hiyo.