NA JAFFAR ABDALLA, PEMBA

VIJANA wametakiwa kuendeleza vipaji vyao, ili kuwa na  mafanikio, kwani kufanya hivyo kutawarahisishia kupata ajira kwa haraka kupitia sekta hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa na kocha mkuu wa timu ya Chipukizi  Mzee Ali Abdalla, alipokuwa akifungua michuano ya  Marco Mbuzi Cup, huko katika kiwanja cha Tibirinzi Wilaya ya Chake chake.

Alisema kuna fursa nyingi za ajira kupitia michezo, hivyo vyema vijana wenye vipaji kuchangamkia fursa hizo.

“Wapo wengi ambao wamefanikiwa kupitia sekta hii ya michezo, walikuwa na vipaji kiasi ambacho hawakutaka kuhimizwa katika mazoezi, hivyo nakuombeni vijana fuateni nyao zao”alisema.

Kwa upande wake muanzilishi wa michuano hiyo Ali Miraji Marco, alisema alishindwa kustahamili baada ya kuona vijana wengi wanaranda mitaani na kuamua kuanzisha michano hiyo.

Aliwataka wadau wa michezo na viongozi kuanzisha michano ya aina kama hiyo ambayo mwisho wa siku ndio inayotoa wachezaji wa madaraja mbali mbali.

Aidha katika michuano hiyo mshindi anatarajiwa kubeba Mbuzi wawili  mshindi wa pili mbuzi mmoja na mshindi wa tatu atazawadiwa shilingi 50,000.