HIVI karibuni, Marekani ilitangaza kumuwekea vikwazo mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC), Fatou Bensouda, huku taifa hilo likitoa maelezo ya kashfa dhidi ya mahakama hiyo.

Taarifa kutoka nchini Marekani zilieleza kuwa rais wa nchi hiyo tayari ameidhinisha vikwazo vya kiuchumi na marufuku ya kusafiri nchini Marekani dhidi ya maofisa wa ya ICC.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo, alisema vikwazo hivyo pia vinalenga familia zao na watu wao wa karibu na maofisa hao wa ICC.

“Hatuwezi kukaa kimya wakati watu wetu wanatishiwa na mahakama isiyofaa na hatutokubali”, alisema Pompeo.

“Kwanza, tunatoa idhini ya kuchukuliwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya maofisa wa ICC wanaohusika moja kwa moja katika uchunguzi wa maofisa wa Marekani na washirika wake bila idhini ya nchi hizo, na dhidi ya wale ambao wanaunga mkono kifedha shughuli hizo za uchunguzi. Vikwazo vitachukuliwa kesi kwa kesi dhidi ya watu au nchi maalum”, alisema.

Pompeo alisema Marekani haitokubali kutoa visa kwa wale wanaohusika moja kwa moja katika uchunguzi huo na vikwazo hivyo pia vitachukuliwa dhidi ya familia zao.

Kwanini Marekani imekuja na hatua ya kumuwekea vikwazo Fatou Bensouda na baadhi ya maofisa wa ICC? Hali hiyo inatokana na mahakama hiyo kufikia hatua ya kuanza uchunguzi dhidi ya makosa ya jinai kwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan na Palestina.

Vitisho vya utawala wa Trump kwa mahakama ya ICC vimekuepo tangu mwaka wa 2018, hata hivyo vitisho hivyo havijazuia uchunguzi kuhusu uhalifu uliofanywa na jeshi la Marekani na shirika la ujasusi la CIA nchini Afghanistan.

Hata hivyo kutokana na ICC hivi sasa kuvalia njuga uchunguzi, Marekani imeshituka na baada yake kuanza kuisema vibaya mahakama hiyo kwa kuiita kuwa ni mahakama ya kifisadi.

Pompeo ameiita mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, kuwa ni taasisi ya kifisadi na Washington inalaani uchunguzi wa mahakama hiyo ya kimataifa unaolenga wanajeshi wa Marekani waliopelekwa nchini Afghanistan.

Mnamo mwezi Aprili mwaka 2020, Marekani ilimnyima viza mwendesha mashtaka wa ICC ya kuingia nchini humo, hata hivyo, ICC imetupilia mbali uamuzi wa Marekani kutangaza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya maofisa wa ,ahakama hiyo wanaochunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kutekelezwa na wanajeshi wa Marekani nchini Afganistan.

Mkuu wa ICC, O-Gon Kwon, alisema mahakama hiyo imebaini kuwepo kwa hatua hizo zinazuia juhudi mahakama hiyo kupambana na tabia za kutowaadhibu wahalifu na kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimishwa duniani kote.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, imeeleza kuwa, kitendo hicho ni dharau kwa waathirika wa makosa ya uhalifu yaliyofanyika nchini Afganistan na majeshi ya Marekani.

Marekani imeikosoa mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa na ni miongoni mwa mataifa mengi ambayo hayajatia saini mkataba wa raia wake kushtakiwa na mahakama hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza jana kuwa Marekani imeweka vikwazo dhidi ya mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Fatou Bensouda kwa sababu ya ofisi yake kuendelea na uchunguzi wa watu wa Marekani.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ndiye alitangaza uamuzi huo ambao haujawahi kutokea. Mike Pompeo amesema ni “muhimu kuanza kuchukuwa hatua dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu”.

“Leo tunaamua kuchukuwa hatua! Marekani haijawahi kutia saini kwenye Mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo ya kimataifa, na hatutavumilia vitimbi vyake visivyokubalika kuwaweka Wamarekani chini ya mamlaka yake, ” ameongeza waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Washington imeamua kumuweka mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda, na pia mmoja wa washirika wake Phakiso Mochochoko kwenye orodha nyeusi. Vikwazo vya kiuchumi pia vimechukuliwa dhidi yao. Hatua ambazo zinaweza pia kuathiri mtu yeyote ambaye anashirikiana na mwendesha mashtaka, amesema Mike Pompeo.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya, katika ofisi ya Mkuu wa Sera za Kigeni Josep Borrel, Peter Stano anasema “Mahakama ya ICC inakabiliana na changamoto za nje za kupingwa na Umoja wa Ulaya unasimama imara dhidi ya majaribio ya kunyong’onyesha mifumo ya kimataifa kufanikisha haki ya jinai kwa kuzuia utendaji kazi wake”.

Aidha akielezea zaidi wakati alipozungumza na waandishi wa habari alisema umoja huo umejiweka madhubuti kuongeza uungaji mkono wao kwa ICC kwa sababu hiyo ni nyenzo muhimu katika makabiliano ya wakwepa mikono ya sheria.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ametangaza kuwa Uingereza vilevile imesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na Marekani dhidi ya maofisa wa ICC.

Shirika la kutetea haki za binaadamu limesema hatua ya utawala wa Rais Donald Trump kuweka vikwazo kwa waendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inaonyesha kupuuzwa vibaya wahanga wa uhalifu mkubwa duniani.

Mkurugenzi wa haki za kimataifa wa Human Rights Watch, Richard Dicker alisema matumizi mabaya ya utawala wa Trump kuweka vikwazo, umeundwa kwa wanaoshukiwa kuwa magaidi na wafanyabiashara wakuu wa dawa za kulevya.

Dicker alisema adhabu hiyo dhidi ya waendesha mashtaka wa uhalifu wa kivita inaonyesha kutowajali waathirika. Shirika hilo limesema amri ya rais ya mwezi Juni imeundwa sio tu kwa ajili ya kuwatisha maofisa na wafanyakazi wa mahakama hiyo wanaohusika na upelelezi muhimu, bali pia kudhoofisha ushirikiano mpana na ICC.

Katika kujibu amri ya rais ya mwezi Juni, nchi 67 wanachama wa ICC, wakiwemo washirika wakuu wa Marekani, walitoa taarifa ya pamoja kuelezea msimamo wao wa kuiunga mkono mahakama ya ICC kama taasisi iliyo huru na isiyoyumbishwa.

Hii iliambatana na taarifa kutoka katika Umoja wa Ulaya, watetezi wa haki za binadamu na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Marekani na ulimwenguni kote. Nchi wanachama za ICC zimerudia mara kadhaa kusisitiza kuiunga mkono mahakama hiyo.

”Wanachama wa ICC wameungana pamoja kabla ya kusimama na waathirika na kutetea mamlaka ya mahakama hiyo kutokana na mashambulizi yasiyo na kanuni, ikiwemo kutoka kwa Marekani,” alisema Dicker.

Alisema serikali hizo zinapaswa kuwa tayari kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mahakama ya ICC inabaki kwenye mkondo wake, ili asitokee mtu yeyote, hata ziwe nchi zenye nguvu ambaye atakuwa juu ya sheria.

Kwa sababu ofisi ya mwendesha mashtaka ya Mahakama ya ICC inalitathmini ombi la Afghanistan na kwa sababu ya vikwazo zinavyohusiana na janga la COVID-19, mahakama hiyo kwa sasa haiendelei na uchunguzi wowote ule nchini humo.