WASHINGTON,MAREKANI

MIEZI michache baada ya Marekani kuamua kulikatia misaada yote ya kifedha Shirika la Afya Duniani kwa madai kwamba linadhibitiwa na China, sasa utawala wa Donald Trump umeenda mbali zaidi ya kuainisha tarehe ya kujiondoa WHO.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani ilitangaza Julai 6 mwaka ujao 2021 kama tarehe rasmi ya kujiondoa nchi hiyo katika taasisi hiyo muhimu zaidi ya afya duniani.

Washington inadai kuwa ilichukua hatua hiyo kwa kuwa WHO imefeli katika utendaji kazi wake ndani ya miongo kadhaa iliyopita, hususan katika kukabiliana na janga la corona.

Marekani ilisema fedha ilizolikatia shirika hilo itazielekeza katika kulipa malimbikizo ya madeni yake katika taasisi nyenginezo za Umoja wa Mataifa.

Baada ya kuongezeka hitilafu na vita vya maneno baina ya Serikali yake na shirika la WHO na kudai kuwa shirika hilo linaipendelea China, hatimaye Trump mwezi Aprili mwaka huu alitoa amri ya kukatiwa shirika hilo mchango wa fedha wa Marekani.

Hii ni katika hali ambayo shirika hilo linahitaji sana msaada huo kwa ajili ya kupambana na kasi ya kuenea virusi hivyo duniani.

Washington ambayo imekuwa mchangiaji mkubwa zaidi wa bajeti ya shirika la WHO ilidai kuwa shirika hilo lilichelewa kuitaarifu Marekani kuhusu mripuko wa ugonjwa wa Covid-19 na daima linaipendelea China.

Hatua hiyo ya Trump ya kuendelea kuiondoa US katika taasisi muhimu za kimataifa ilikabiliwa na lawama kali za ndani na nje ya nchi.