WASHINGTON,MAREKANI

WAZIRI wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo alitangaza  kuwa Marekani imeweka vikwazo dhidi ya mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Fatou Bensouda kwasababu ya ofisi yake kuendelea na uchunguzi wa watu wa Marekani.

Pompeo alisema aliyeongezwa pia katika orodha ya vikwazo ni Phakiso Mochochoko mkuu wa idara ya sheria ya ICC, anayehusika na ushirikiano na hisani, kwa kutoa msaada kwa Bensouda za taarifa mbali mbali.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani aliita mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita, ambayo Marekani haihusiki nayo, kuwa ni taasisi iliyovurugika na yenye ufisadi wa hali ya juu.

Mwezi Juni,Rais wa Marekani Donald Trump alitoa amri ya rais inayoweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya maofisa wa ICC wanaohusika katika uchunguzi wa vikosi vya jeshi la Marekani kwa uwezekano wa uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.