NA MWAJUMA JUMA

MICHUANO ya soka ya Zanzibar Veterani inatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake leo Ijumaa, kwa mchezo utakaowakutanisha Klachi mbovu na Dimani, ambao utapigwa uwanja wa Mao Zedong au Fuoni.

Michuano hiyo ambayo itashirikisha timu saba itachezwa kwa mtindo wa ligi na zimepangwa katika makundi mawili, itakuwa ikichezwa siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu Msaidizi wa kamati ya mashindano hayo Abdalla Ali Mohammed, alisema mpaka jana ni timu saba pekee ndio zilimethibitisha kushiriki.

 Alisema mashindano yao ni ya kwanza kufanyika hivyo yatakuwa na changamoto nyingi, ambazo kama kamati wanajipanga kuzikabili.

 Timu ambazo zinashiriki ligi hiyo ni KVZ, Dimani, Klachi mbovu, Mafunzo, Kijichi, Vitumbo na timu ya Mlandege Veteran ambazo kwa mujibu wa kanuni ya mashindano hayo, mchezaji atanayeruhusiwa kucheza kuanzia umri wa miaka 35 na kuendelea na asiwe anashiriki ligi yoyote inayoandaliwa na FA.