YAUNDE,CAMEROON
MASHIRIKA ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya mahakama nchini Cameroon kuwapa adhabu nyepesi wanajeshi waliopatikana na hatia ya kuua raia akiwemo mtoto mdogo.
Awali Serikali ilikanusha madai kuwa askari hao saba walihusika na mauaji ya raia wanne katika eneo la Zeleved la kaskazini mwa nchi mwaka 2015, lakini wakakamatwa baadaye baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kuwasilisha ushahidi wa video dhidi yao na kesi hiyo ikafunguliwa Januari mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa haki katika eneo la Afrika ya Kati Maximilienne Ngo Mbe,aliitaja hukumu iliyotolewa na mahakama ya Cameroon dhidi ya askari hao kama dhaifu na isiyo na maana.
Wanne miongoni mwa askari hao walihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela,mwengine alifungwa miaka miwili jela, huku wawili wakiachiwa huru.
Video iliyosambaa mitandaoni Julai mwaka 2018, ilionyesha wanajeshi hao wakiwapiga risasi kwa nyuma wanawake wawili waliokuwa wamefungwa macho huku wakiwa wamepiga magoti, na kisha kuua mtoto mdogo aliyekuwa mgongoni mwa mwanamke mmoja na msichana.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki katika eneo la Afrika ya Kati alisema hukumu ya miaka kumi jela si tu dhaifu, lakini pia haina maana yoyote.
Hukumu hiyo haina umuhimu kwa kuwa walioua sio waliotoa agizo la kutekelezwa mauaji hayo.
Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliwatuhumu maofisa usalama wa Cameroon kwamba walihusika na mauaji ya raia 22 wakiwemo watoto wadogo 13 na wanawake wawili wajawazito mnamo Februari 14 katika jimbo linalozungumza Kiingereza.