KAMPALA,UGANDA

KIWANGO  cha mauzo ya nje ya dhahabu nchini Uganda kimeongezeka hadi kufikia mauzo ya thamani ya dola milioni 160 ndani ya mwezi wa Juni pekee,suala lililozusha mjadala.

Zliibuka tuhuma kuhusu vyanzo halisi vya dhahabu hiyo kama ni halali au inatoka mataifa ya jirani na nchi hiyo.

Mwezi uliopita Benki ya dunia ilikadiria kiwango cha dhahabu haramu ya thamani ya dola milioni moja kilichosafirishwa kibiashara kupitia Uganda.

Inadaiwa pia kuwa kutokana na janga la covid19, wafanyabishara wa magendo wanatumia ndege za kukodisha kusambaza vifaa vya huduma za afya kusafirisha dhahabu za magendo.

Kamishina wa wizara ya madini Vincent Kedi alisema Serikali ya Uganda ilikiri kuwa haiwezi kuzalisha kiasi kikubwa kama hicho, lakini kuwepo kwa mitambo ya kusafisha dhahabu kunasababisha kuwepo kwa kiwango cha juu.

“Kiwango cha uzalishaji wa dhahabu nchini Uganda kiliongezeka ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita, pia tuna viwanda vitano vya kusafisha dhahabu hapa nchini, na hivi vinasafisha dhahabu ya ndani na kutoka nje ya nchi hivyo usafirishaji wa dhahabu uliongezeka kutokana na hilo.”alisema.

Kedi alikana kuwepo dhahabu ya magendo kutoka mataifa jirani kama vile DRC ndiyo ilisababisha kuongezeka kwa usafirishaji zaidi.

Aidha naibu wa mwenyekiti wa kampuni ya AGR Alphonse Katarebe alisema tangu kuanzishwa kwa Kampuni za kusafisha dhahabu nchini Uganda,kiwango cha uzalishaji kimepanda.

Licha ya kuwa Uganda haina migodi mikubwa ya dhahabu, hivi karibuni madini yalikuja kuwa mojawapo ya bidhaa kwa masoko ya nje zinazoiletea fedha nyingi za kigeni hata kuliko zao la kahawa.

Hali hii ilileta ushindani mkali miongoni mwa wanaoshiriki biashara hiyo huku wawekezaji kadhaa wakianzisha mitambo ya kusafisha dhahabu nchini ambako dhahabu huandaliwa kwa soko la kimataifa.