NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Mfenesini imetwaa ubingwa wa michuano ya soka ya Baraza la Vijana wilaya ya Magharibi A kwa kuifunga Welezo B kwa penanti 18-17.

 Miamba hiyo iliyoshuka katika dimba la Regeza Mwendo ililazimika kupigiana penalti, baada ya kumaliza dakika 90 wakiwa wamefungana bao 1-1.

 Katika mchezo huo ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud ambae alikabidhi zawadi kwa washindi hao.

 Mfenesini ilistahili kupata ubingwa huo kutokana na kuonesha uwezo wao wa hali ya juu katika idara zote za mchezo huo ambao ulitoa burudani tosha machoni mwa mashabiki waliokuwa wakiangalia mchezo huo.

Mfenesini katika mchezo huo bao lao lilifungwa na mchezaji Hemed Zubeir dakika ya pili na la Welezo B lilifungwa na Iddi Idrissa dakika ya 49.

Katika fainali hiyo bingwa alipata zawadi ya kikombe, shilingi 1,000,000 na mpira mmoja wakati mshindi wa pili alipata shilingi 200,000 na mpira mmoja.

Aidha katika fainali hiyo zawadi mbali mbali zilitolewa ikwiemo kwa mchezaji bora wa mchezo huo wa fainali  Hassan Said wa timu ya Welezo, na mchezaji bora wa mashindano alikuwa ni Hemed Zahran wa Mfenesini, zawadi ya mlinda mlango bora ilikwenda kwa Mudathir Ali Makame wa timu ya Bububu B.