NA SAIDA ISSA, DODOMA
CHUO Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kimetoa ripoti ya tathmini ya mfumo wa kieletroniki katika ukusanyaji mapato na usimamizi wa fedha za umma (GePG), ambayo imeonesha kuwa hali ya ukusanyaji mapato imeongezeka.
Akiwasilisha ripoti hiyo jijini Dodoma, Mhadhiri kutoka Chuo cha Tehama cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (CoICT) Prof. Joel Mtebe alisema ripoti hiyo imeonesha kwamba asilimia 77 ya watu waliojiwa wamesema kwamba mfumo huo umeisaidia serikali kuongeza mapato yake,
“Mojawapo ya sababu ilikuwa ni gharama zilizokuwa zikutumiwa katika ukusanyaji kulipa taasisi mbalimbali. Lakini kuongezeka kwa mapato kumesababishwa na watu kulipia kwa njia ya simu pamoja na benki,” alisema.
Alisema asilimia 87 ya watendaji waliohojiwa walisema kwamba mfumo huo umewasaidia kuweza kukusanya mapato ya serikali.
“GePG imeweza kupunguza gharama kubwa ambazo zilikuwa zikitumiwa awali pia tulipitia ‘document’ za makusanyo kuangalia gharama wanazotumia, gharama zilizokuwa zikitumia 2017 zilikuwa juu lakini kwa sasa zimepungua. Kuna punguzo la asimilia 27 za gharama ambazo taasisi za serikali zilikuwa zikitumia kukusanya maduhuli za Serikali”, alisema.
Alisema walitumia vigezo vitatu kujua ubora wa mfumo ambavyo ni ubora, ubora wa ripoti pamoja na ushirikiano wanaupata kutoka kwa watendaji wa mfumo.
“Kwa lugha rahisi katika vigezo vitatu tulivyotumia ambavyo tuliwahoji wananchi au watumiaji wa mfumo umeonesha kitu ambacho kinachangia waridhike na mfumo ni ubora wa ripoti wanaamini ripoti zina data na ubora”.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema mfumo huo ulianzishwa Julai mwaka 2017 ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo Serikalini katika zoezi la ukusanyaji wa fedha za umma.
Katibu Mkuu huyo alisema mfumo huo umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani wa Serikali ambapo upo kwa mujibu wa sheria ya fedha za umma.
Alisema kuanzishwa kwa mfumo huo kumeleta faida mbalimbali ambazo ni kuongezeka kwa uwazi na udhibiti wa katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo, kuwa na viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa fedha za kuchochea ubunifu.