KABUL,AFGHANISTAN
MSHAURI wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna ufumbuzi wa kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan.

Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya Asia Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Rasoul Mousavi, alisema mgogoro wa Afghanistan unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa pekee.

Rasoul Mousavi

Mousavi alisema hayo jana katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa,hakuna ufumbuzi wa kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan, lakini ieleweke kuwa, ufumbuzi wa kisiasa hautafuata malengo yaliyo sawa na ya kijeshi.

Aliongeza kuwa, utatuzi wa kisiasa ni msamaha na mapatano kwa maslahi ya taifa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran aliashiria kuhusu mazungumzo ya Waafghanistan yanayofanyika mjini Doha Qatar na kubainisha kuwa, anatumai mkutano huo utapelekea kupatikana amani na uthabiti nchini Afghanistan ili wakimbizi wa Kiafghani popote walipo duniani, waweze kurejea nyumbani kwa fahari.

Alisema kuanza mazungumzo ya Doha kuhusu mustakabali wa Afghanistan kumesadifiana na kuanza kwa zoezi la kuwatambua raia wa Afghanistan wanaoishi nchini.Iran ni mwenyeji wa mamilioni ya wakimbizi wa Kiafghani.

Duru ya kwanza ya Mazungumzo ya Waafghanistan (IAN) iling’oa nanga mjini Doha kwa kuhudhuriwa na Mike Pompeo,Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, maofisa wa Serikali ya Qatar, na wawakilishi wa nchi 30 duniani.