NA AHMAD MAHMOUD, ARUSHA

CHAMA cha Siasa cha ADA-TADEA kimezindua kampeni zake za ubunge katika jimbo la Arusha mjini na kueleza kuwa kipaumbele chake ni kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya akina mama na vijana, ili iwasaidie kuanzisha miradi mbalimbali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.

Kampeni hizo, zilizinduliwa jana katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani jijini hapa ambapo Mgeni  rasmi Nuru Kimwaga, ambaye ni Katibu wa Itikadi na uenezi wa chama hicho Taifa alimnadi mgombea ubunge wa chama hicho Zuberi Mwinyi na kuwataka wana Arusha kumchaguaAkizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kimwaga alisema kuwa jiji la Arusha linatakiwa kuwa na mbunge mchapakazi, mkweli, mwadilifu na  mwaminifu na Zuberi Mwinyi ndio chaguo sahihi la wana Arusha kwani  kwa kipindi kifupi tulichokuwa naye ADA-TADEA wameona uwezo wake.

Mgombea ubunge huyo akinadi sera zake amesema  kuwa atajenga jengo la kisasa kwa ajili ya machinga kwani wanapaswa kuwa na eneo lao maalumu la kufanyia shughuli zao.

 Mgombea huyo, ameahidi kuwapatia akina mama wajasriamali mikopo ya shilingi milioni 2 isiyo na riba, ili kuinua miradi yao  na kutoa pikipiki maarufu bodaboda za bei nafuu kwa vijana, ili waweze kujiajiri.