NA HAJI NASSOR

MGOMBEA uwakilishi wa jimbo la Mtambile kupitia chamacha wananchi CUF, Asha Said Suleiman, amesema akipata ridhaa ya wananchi kuliongoza jimbo hilo, ataanza kulishughulikia tatizo la udhalilishaji jimboni humo.

Alisema, anakosa usingizi na kuumizwa mno jinsi wanawake na watoto wanavyodhalilishwa na kisha kushindwa kuzisimamia kesi zao, kufika mahakamani.

Alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, juu ya ahadi zake kwa wananchi pindi wakimpa ridhaa kushika nafasi hiyo.

Alisema amejipanga kuwatafutia mwanasheria na kuanzisha kamati maalum ya jimbo, ambayo itakuwa inashughulikia suala hilo pekee, kwa lengo la kuhakikisha  watato wanaodhalilishwa wanapata haki zao.

Alisema haingii akili kuona familia iliyokumbwa na ubakaji

mtoto wao wanakosa ushirikiano na mamlaka husika na kisha kesi hiyo kuishia kituo cha polisi kwa kukosa mwanasheria wa kuifuatilia.

“Mimi naomba wapiga kura wa Jimbo la Mtambile, wanipe kura kwa wingi hapo Oktoba 27 na Oktoba 28 mwaka huu, na nikishinda kipaumbele changu ni kuhakikisha udhalilishaji unakoma jimbo la Mtambile,’’alisema.

Aidha, alisema wananchi wakikubali kumpa ridhaa, atahakikisha anaimarisha ajira za sekta binafsi kwa wanawake na vijana.

Alisema, eneo la Kisiwa panza wapo wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, ingawa hawaoni faida kubwa, kutokana na kukosa namna ya kuusarifu mwani huo.

“Nimepanga kuwaletea mtalaamu, ili wakimaliza kuvuna mwani, watengeneze vileja, makwaru, chauro na chipsi na hata sabuni na mafuta, ili waongeze pato lao,”alieleza.

Hata hivyo, alisema atawapatia vijana na wanaume wengine mtaalamu wa upishi wa chumvi ya mawe, kwa vile ina soko kubwa hapa visiwani.