NA MWAJUMA JUMA

MHADHIRI kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Profesa, Issa Haji Ziddy, ameitaka Jamii ya Kizanzibari kutambuwa hakuna sehemu yoyote inayomkataza au kumzuia  mwanamke kutokuwa kiongozi kwa misingi ya dini.

 Prf. Ziddy, aliyasema hayo  alipokua akizungumza na viongozi wa dini mbali mbali na baadhi ya wawakilishi kutoka asasi za kiraia huko katika ukumbi wa Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar),  uliopo Tunguu Wilaya ya kati Unguja, wakati wa uwasilishwaji wa muongozo wa utowaji wa elimu dhidi ya nafasi ya mwanamke na uongozi katika Uislamu.

Alisema kwa miaka mingi wanawake  visiwani Zanzibar wamekua wakipoteza fursa za uongozi kutokana na baadhi ya watu kwenye jamii kuwa na dhana potofu ikiwemo kuamini kuwa mwanamke hapaswi kuwa kiongozi jambo ambalo halina ukweli.

“Tunaingia katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, katika uchaguzi huo kuna wanawake na wanaume ambao wamechukuwa fomu kuomba nafasi mbali mbali za uongozi sasa isiwe watu wanapita na kuanza kusema maneno kwa misingi ya dini”, alisema.

Alisema  wapo baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao wanatumia baadhi ya aya za Qur-an kuwakandamiza wanawake na kupelekea wanawake hao kupoteza fursa ambazo anaamini zingeweza kuwakomboa wao na familia zao.

‘’Watu wanasahau kuwa katika mkataba wa hudaibiya ushauri wa makubaliano yale kwa mara ya kwanza ulitoka kwa mwanamke ambae alikwenda kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na wengi wa wanaume wakiwemo maswahaba walidhani wanakandamizwa lakini ulikua mwanzo wa kheri kwa  dini ya kiislamu.’’alifahamisha.

Prf. Ziddy ,alishangaa kuona pamoja na mifano hai ya ndani ya dini, lakini bado  kuna kundi kubwa la wanajamii wanaendelea kuamini kuwa kazi za mwanamke ni kutunza familia na wengine hawaruhusiwi hata kuwa viongozi kwenye mikutano ya familia zao.

Nae Mjumbe wa Kamati ya Amani Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alisema si sahihi wanawake kunyimwa fursa hizo na kuwa wanaofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa wanabeba dhima na wanapaswa kuacha mara moja.

Hivyo aliwataka wanawake visiwani hapa kubadilika na kukataa kabisa kujidhalilisha wenyewe na kusema kuwa ni chanzo kikubwa ambacho wanaume hukitumia kama fursa kuwakandamiza.

Kwa upande wake Father Stanley Nicholas, kutoka kanisa la Angilaka Mkunazini mjini Unguja alisema yanayoendelea kutokea yote ni kwa sababu ya watu kutokua na elimu na kukosa utayari wa kujifunza.

Alisema watu wengi katika jamii wanaamini elimu ya dini ni ile walioikuta, lakini wanashindwa kujiongeza kusoma zaidi ambapo anaamini wangeweza kupata mwanga na kuona uhalisia ulivyo.

Nae Amina Salum Khalfan alisema inasikitisha sana kuona hata Baraza la Maulamaa kisiwani hapa kukosa ushiriki wa wanawake, jambo ambalo anaamini ni kuendeleza mfumo dume.

Alisema kuwa Baraza la Maulamaa ni baraza ambalo linafanya kazi ya kuhudumia jinsia zote hivyo kuna kila sababu ya ushiriki wa wanawake ndani yake, kitu ambacho hakikifanyika licha ya wanaharakati kupaza sauti zao.